Makamu wa Rais Dk. Ali Mohamed Shein amesema Watanzania wanapaswa kuunga mkono jitihada za serikali katika kuitangaza Tanzania ili kuweza kupata wawekezaji wa kuja kuwekeza nchini.
Akizungumza na Jumuiya ya Watanzania wanaoishi New Dehli , India jDk. Shein alisema suala la kuitangaza Tanzania na vivutio vyake ni la watu wote na wala si la kuiachia serikali pekee.
“Kuitangaza Tanzania ni suala la kila mmoja wetu kwa mujibu wa nafasi zao”, alisisitiza Makamu wa Rais.
Alisema lengo la serikali ni kuwa na wawekezaji wengi nchini ili kuweza kuinua uchumi wa Taifa na kwamba lengo hilo litafanikiwa tu endapo watanzania na hasa wanaoishi nje ya nchi wataunga mkono jitihada hizo za kuitangaza Tanzania nje ya mipaka yake.
Akizungumzia hali ya nyumbani kwa ujumla Dk. Shein aliwaambia watanzania hao kuwa ni shwari na kuna utulivu na watu wanaendelea na shughuli zao za kujiletea maendeleo.
Kuhusu chakula alisema pamoja na kutokuwa na mvua za kutosha za vuli hakutakuwa na shida ya chakula kwa kuwa serikali imeagiza wafanyabiashara kuagiza chakula kama vile mahindi kutoka nje ya nchi na kusisitiza kilichopo kitunzwe.
Suala la muafaka alisema mazungumzo kati ya Chama Cha Mapinduzi CCM na Chama Cha Wananchi CUF yanaendelea na yamefikia katika hatua kubwa na kwamba muda ukifika makatibu wakuu wa vyama hivyo wataeleza hadharani.
Dk. Shein alitumia fursa hiyo pia kuwataka Watanzania kuwekeza nyumbani jambo ambalo litawasaidia katika siku za baadaye.
Dk. Shein pamoja na shughuli nyingine jioni hii anatarajiwa kufungua mkutano wa ushirikiano wa kibiashara kati ya India na Afrika ( India - Africa project Partnership Conclave).

Habari kwa hisani ya Penzi Nyamungumi
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: