Na Hamida Ramadhan – Dodoma.
Dodoma, Julai 29, 2025 – Zikiwa zimesalia chini ya miezi mitatu kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, hali ya taharuki na matarajio imetawala Makao Makuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mjini Dodoma, kufuatia kucheleweshwa kwa kutangazwa kwa majina ya wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi kupitia chama hicho tawala.
Kwa zaidi ya saa 18 mfululizo, Ukumbi wa NEC uliopo katika jengo la White House – Makao Makuu ya CCM – umekuwa kitovu cha shughuli, minong’ono, na hali ya kusubiri isiyoisha, huku waandishi wa habari na wadau wa siasa wakipiga kambi nje ya ukumbi huo kwa matumaini ya kusikia orodha rasmi ya wagombea.
Awali, taarifa kutoka chama zilisema kikao cha Kamati Kuu, kilichotarajiwa kuongozwa na Katibu wa NEC – Itikadi, Uenezi na Mafunzo, CPA Amos Makalla, kingefanyika Julai 28 saa 11 jioni. Hata hivyo, muda huo ulipita bila kikao kufanyika, na bila maelezo ya moja kwa moja kutolewa kwa umma.
Hali hiyo ilisababisha sintofahamu miongoni mwa wanahabari waliokusanyika eneo hilo, ambapo wengi walilazimika kusubiri hadi usiku wa manane wakiwa na matumaini ya kupata taarifa. Hata hivyo, hadi alfajiri ya Julai 29, tangazo hilo bado halikuwa limetolewa, na badala yake walielekezwa kuwa kikao kingeendelea saa 4 asubuhi.
Wakati huo ukifika, bado taarifa hazikutolewa, na muda mwingine wa saa 6 mchana ukatangazwa kwa kuendelea na vikao vya ndani – hali iliyoibua maswali miongoni mwa wachambuzi wa siasa kuhusu sababu halisi za kucheleweshwa kwa tangazo hilo muhimu.
Taarifa zisizo rasmi kutoka ndani ya chama zinaeleza kuwa ucheleweshaji huo umetokana na kazi ya kina ya uhakiki wa mwisho wa majina ya wagombea, ikiwemo kupitia mapendekezo kutoka vikao vya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) na Kamati Kuu (CC).
CPA Makalla anatarajiwa kutoa taarifa rasmi kwa vyombo vya habari mara baada ya kukamilika kwa kikao hicho cha ndani, ambapo anatarajiwa kutangaza majina ya wagombea wa Ubunge wa Majimbo Tanzania Bara, Viti Maalum vya Wanawake, pamoja na wagombea wa Baraza la Wawakilishi visiwani Zanzibar.
Hadi kufikia saa za mchana leo, hali ndani na nje ya White House imeendelea kuwa ya utulivu lakini yenye mvutano wa kimyakimya, huku wanahabari wakifuatilia kwa karibu kila mabadiliko ya mazingira na mienendo ya viongozi waandamizi wa chama.
Wadau wa siasa wameeleza kuwa orodha hiyo inatarajiwa kutoa taswira ya mwelekeo mpya wa CCM kuelekea kampeni za Uchaguzi Mkuu, na huenda ikawa na athari kubwa kwa mikakati ya vyama pinzani nchini.
Huku wananchi wakifuatilia kwa karibu kupitia televisheni, redio, na mitandao ya kijamii, CCM imeendelea kusisitiza kuwa mchakato wa uteuzi wa wagombea unazingatia misingi ya haki, uadilifu, uwezo wa uongozi, ushawishi katika jamii na ushindani wa kisiasa katika maeneo mbalimbali.
“Tunahakikisha tunachagua wagombea wanaokidhi matarajio ya chama na wananchi. Hii ni kazi kubwa na ya kuzingatia kwa makini,” alisema mmoja wa viongozi wa chama ambaye hakutaka kutajwa jina lake.
Kwa sasa, macho na masikio ya wengi yameelekezwa Dodoma, wakisubiri sauti rasmi ya chama tawala kueleza ni nani watakaobeba bendera ya CCM katika uchaguzi wa kihistoria unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29 mwaka huu.



Toa Maoni Yako:
0 comments: