WASANII mbalimbali wanatarajia kutoa burudani katika tamasha la kupinga ujangili dhidi ya Tembo, linatakalofanyika Jumamosi kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja Dar es Salaam.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mratibu wa kampeni hiyo, Asukile Kajuni, alisema kuwa tamasha hilo limeandaliwa na taasisi ya sanaa ya Nafasi Art Space.
Alisema kuwa tamasha hilo linatarajiwa kufanyika kwa mara ya kwanza Dar es Salaam ambapo baadaye litakuwa endeevu nchi nzima.
Mratibu huyo alisema kuwa wameamua kuanzisha kampeni hiyo kwa ajili ya kupiga vita ujangili dhidi ya Tembo unaoendelea katika misitu mbalimbali nchini kwa kupitia sanaa.
“Kwa kupitia sanaa tunatarajia kufikisha ujumbe kirahisi kwa jamii ili kuweza kutokomeza ujangili unaoendelea dhidi ya Tembo kwa manufaa ya watanzania wote,” alisema.
Naye msanii wa kundi la Wahapahapa, Paul Ndunguru alisema kuwa watatembea na Tembo aliyetengenezwa na wasanii hao kwa ajili ya kuhamashisha kutokomeza ukatili huo dhidi ya Wanyama.
Alisema kuwa wameamua kujipanga kutokomeza ukatili wa wanyama kwa kupitia nyimbo zao na sanaa mbalimbali za mikono.
“Tumejiandaa vizuri na lengo letu kubwa ni kutoa burudani pamoja na ujumbe kwa jamii kwa ajili ya kutokomeza ujangili dhidi ya wanyama,” alisema.
Wasanii wengine watakaotoa burudani ni pamoja na Jikhoman, T Africa, Baba Watoto pamoja na kikundi cha maonyesho ya sanaa za uchoraji.
---



Toa Maoni Yako:
0 comments: