Mkutano wa kilele kati ya Umoja wa Afrika-AU na Uturuki ulimalizika hapo juzi mjini Istambul Uturuki ambapo viongozi hao walipitisha Azimio la Ushirikiano la Istambul pamoja na Mkakati wa Namna ya Utekelezaji wa Ushirikiano huo.

Katika mkutano huo Makamu wa Rais Dk Ali Mohammed Shein ambaye alimuwakilisha Rais Kikwete alisisitiza ndani ya ushirikiano huo umuhimu wa kubuni miradi inayotekelezeka na kutekelezwa kwa wakati ili kuhakikisha malengo ya ushirikiano huo yanafikiwa.

Dk Shein alibainisha kuwa suala muhimu la kuzingatia katika ushirIkiano huo si kuwepo au kutokuwepo kwa fursa za kushirikiana bali zaidi ni namna ushirikiano huo utakavyoweza kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya wananchi wa bara la Afrika.

Akiwa mjini Istambul Dk Shein alikutana pia na Rais wa Uturuki Abdullah Gul ambapo kwa pamoja walizungumzia nia na dhamira za serikali za nchi zao kuimarisha uhusiano na ushirikiano uliopo ambao waliuelezea kuwa katika hali ya kindugu na maelewano makubwa.

Waliazimia kuuimarisha uhusiano huo ambapo kwa upande wake Rais Abudullah aliahidi kuwa nchi yake itafungua ubalozi wake nchini Tanzania katika kipindi kifupi kijacho wakati Dk Shein alieleza kuwa katika hatua za awali Tanzania itauimarisha ubalozi wake ulioko mjini Roma Italia ili uweze kushughukia kikamilifu maslahi ya Tanzania nchini Uturuki

Akizungumzia umuhimu wa mkutano huo mara baada ya kupitishwa Azimio la Istambul na Mkakati wa Utekelezaji wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Bernard Membe alieleza kuwa Uturuki ni nchi muhimu kiuchumi hivi sasa na ndio maana Umoja wa Afrika umeamua kuchangamkia ushirikiano na nchi hiyo

Waziri Membe ambaye awali aliongoza Kikao cha Baraza la Mawaziri wa AU kilichoutangulia Mkutano huo wa viongozi alieleza kuwa Afrika ikiwemo Tanzania imeelekeza nguvu zake katika kuimarisha mawasiliano ya kibiashara na kiuchumi na nchi hiyo na msisitizo ukiwekwa katika kilimo kwani sehemu kubwa ya uchumi wa Uturuki unategemea kilimo.

Waziri Membe alieleza pia kuwa Tanzania inatarajia kufaidika sana chini ya ushirikiano huo na kupitia uhusiano wake na Ututuki katika ngazi ya nchi na nchi ambao nchi hiyo imeonyesha dhamira na ari ya kushirkiana na Tanzania katika nyanja nyingi.

Mikutano ya aina hii ya ushirikiano kati ya AU na nchi nyingine imeshafanyika ikiwemo India , China na Japan.

Makamu wa Rais alirejea nchini jana mchana.

SA
ALHAMISI 21 AGOSTI 2008
DAR ES SALAAM
Said J K Ameir

PRESS SECRETARY TO THE VICE PRESIDENT
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: