CUBA inajivunia uhusiano na ushirikiano uliopo kati yake na Zanzibar hatua ambayo itaendelezwa zaidi na viongozi wa nchi mbili hizo sambamba na mikakati maalum ya kuimarisha sekta za maendeleo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii nchini.

Kauli hiyo imetolewa na Balozi wa Cuba nchini Tanzania Mhe. Felipe Ruis O’Farril alipofika Ikulu mjini Zanzibar kwa ajili ya kumuaga Rais wa Zanzibar na Mweneykiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Amani Abeid Karume.

Katika maelezo yake Balozi Felipe alimueleza Rais Karume kuwa Cuba itaendelea kushirikiana na Zanzibar sambamba na kuangalia uwezekano wa kuongeza misaada yake katika sekta nyenginezo za maendeleo ambapo kwa upande wa sekta ya afya inaangalia uwezekano wa kuanzisha tawi la mafunzo ya udaktari kisiwani Pemba ambalo walimu wake watakuwa ni madaktari kutoka Cuba.

Adha, Balozi Felipe alieleza kuwa Cuba itafanya taratibu za kuhakikisha inaleta wataalamu wa utunzaji mji Mkongwe sambamba na wataalamu wa wadudu wa mazao ya chakula hasa embe.

Alisema kuwa Zanzibar na Cuba zina historia ya muda mrefu tokea wakati wa Marehemu Mzee Abeid Amani Karume na Rais Fidel Castro pamoja na Ernestro Che Guevara ambapo ipo haja ya kuimarishwa zaidi uhusiano huo uliowekwa na Wanamapinduzi hao ambao una manufaa kwa nchi zote mbili na wananchi wake.

Bwana Felipe alimpongeza Rais Karume, viongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na wananchi wote wa Zanzibar kwa ukarimu na upendo mkubwa walionao kwa ndugu zao wa Cuba sambamba na kupongeza mashirikiano mazuri aliyoyapata Zanzibar katika kipindi chote alichofanya kazi Tanzania.

Aidha, Mhe. Felipe alisema kuwa Cuba imepata mafanikio makubwa katika kuimarisha sekta zake za maendeleo na kusisitiza kuwa itaendelea kuimarisha uhusiano wake ili Zanzibar nayo izidi kupiga hatua kimaendeleo.

Nae Rais Karume alimueleza Mhe. Felipe kuwa wananchi wa Zanzibar wamefarajika kwa kiasi kikubwa kutokana na mashirikiano na mahusiano yaliopo baina ya Cuba na Zanzibar pamoja na kupendezewa na huduma za afya wanazozipata kutoka kwa madaktari wa Cuba.

Rais Karume alimpongeza Balozi Felipe na nchi yake na kueleza kuwa Zanzibar inathamini na inajivunia uhusiano uliopo kati yake na Cuba pamoja na kupongeza utekelezaji wa ahadi za nchi hiyo kwa Zanzibar ikiwemo madaktari wakufunzi kutoka nchini humo waliopo hapa Zanzibar ambao wanaendelea kutoa mafunzo na tiba kwa wananchi.

Dk. Karume alisema kuwa kutokana na utekelezaji wa ahadi hizo inaonesha wazi kufanikiwa kwa mazungumzo kati yake na viongozi wa nchi hiyo akiwemo Makamu wa Rais wa Cuba na Mjumbe wa Kamati Maalum ya Chama cha Kikomunisti cha Cuba ‘CCP’ Bwana Esteban Lazo Hernandez hapo Novemba mwaka juzi mjini Havana, Cuba akiwa ziarani nchini humo.

Rais Karume alisema kuwa Zanzibar inafurahia uhusiano na ushirikiano uliopo kati yake na Cuba hali ambayo imeweza kupelekea kuimarishwa kwa sekta za maendeleo ikiwemo afya na elimu.

Katika mazungumzo hayo Dk. Karume aliipongeza Cuba kwa mafanikio iliyoyapata katika sekta za maendeleo ikiwemo sekta ya afya ambapo hivi sasa imefikia hatua ya kuwa na Daktari mmoja kwa kila Wacuba 600 uwiano ambao unazishinda nchi zilizoendelea duniani.

Balozi Felipe alisema kuwa lengo la Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuanzisha chuo cha madaktari ni zuri na litasaidia katika kutoa huduma ya afya sanjari na kuwasaidia madaktari wazalendo kwenda katika chuo kikuu cha MATANZAS kilichopo nchini humo kumalizia masomo yao, chuo ambacho kinatoa elimu kwa wanafunzi kutoka nchi mbali mbali duniani.

Alisema kuwa Cuba imo katika kujiimarisha zaidi katika kutoa mafunzo kwa kutumia teknolojia ya kisasa hali ambayo itasaida kwa kiasi kikubwa kuzisaidia nchi rafiki wa Cuba ikiwemo Zanzibar.

Habari kwa hisani ya Rajab Mkasaba
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: