Na. Msafiri Ulimali- MAELEZO.

Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein amefanya ziara katika miradi mbalimbali na kutoa maagizo juu ya utekelezaji kwa baadhi ya wizara, ikiwa ni pamoja na kuangazia maeneo kadhaa ikiwemo suala la mazingira.

Ikumbukwe kuwa utunzaji wa mazingira ni kati ya rasilimali rafiki kwa binadamu kwani ikipotea bila shaka uhai nao upo mashakani, Rais Dkt. Shein ametoa tahadhari mapema juu ya kupungua kwa mchanga kisiwani Zanzibar na kuunda tume maalum aliyowajumuisha Mawaziri, Makatibu Wakuu ambao amewapa jukumu la kufikiria njia bora za kuchimba mchanga.

Akikagua maeneo yanayotegemewa zaidi kwa upatikanaji wa rasilmali ya madini ya mchanga katika machimbo ya Pangatupu pamoja na Chechele Dkt. Shein amesema “Mchanga katika mashimo haya umepungua kwa asilimia kubwa jambo ambalo linakwamisha baadhi ya miradi pamoja shughuli za ujenzi za nyumba za wanachi kukwama”.

Aidha, Rais Dkt. Shein, amewaeleza wananchi namna rasilimali ya mchanga ilivyopungua na kutaka wanachi kushirikiana na serikali kupanga mikakati kabambe ambayo itawezesha kutunza rasilimali hiyo ili iweze kutumika kwa uangalifu mpaka pale suluhisho sahihi litakapo patikana.

Akitoa sababu ya kupungua kwa rasilimali hiyo ya mchanga ni pamoja na kutofuatwa kwa sheria za nchi na sasa kuchangia uhaba wa rasilimali hiyo kuwepo visiwani hapo. Pia,wengine wanadaiwa kutumia kama njia ya kujichukulia mchanga bila utaratibu maalum.

Akifafanua kuhusu maeneo hayo Rais Dkt Shein ameongeza kwa kusema kuwa, mashimo ya Pangatupu yakadiliwa kuwa ekari 64, na jumla ya Tani 50,000 zilizobakia na mchanga. Ambapo mashimo ya Chechele yana jumla ya tani 2,000 ambazo zinategemewa kwaajili ya miradi ya serikali kama ujenzi wa Hospitali, shule, Masoko pamoja na ofisi.

Rais Dkt Shein amesema athari zimeanza kuonekana mfano miradi mkubwa kama ujenzi wa jengo la Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (ZURA) umekwama kutokana na ukosefu wa mchanga na jambo hili limepelekea mkakandarasi kusitisha ujenzi mpaka pale atakapopata rasilimali ya mchanga, kwa msisitizo mradi wa ZURA unategemewa zaidi kutoa huduma kwa wakazi wa Zanzibar, ambapo inasimamia miradi mikubwa muhimu.

Vilevile kuna athari za kimazingira kwa kuwa mashimo hayo kipindi cha mvua, yanajaa maji ambayo sio tu yanahatarisha maisha ya watu hususan watoto na wanyama lakini vilevile, yanakuwa mazalia ya mbu na kujenga mazingira ya kuibuka maradhi yakiwemo ya milipuko kama homa ya matumbo ya kuharisha na wakati mwingine kupelekea kipundupindu. Hebu angalia idadi ya watu itakavyoathirika na janga iwapo udhibiti usingetiliwa mkazo. 

Ipo haja ya wafanyabiashara kote nchini kuwasiliana wahusika na kutazama jambo hili kwa mtazamo wa kuokoa mazingira na kuhakikisha shughuli za maendeleo zinatekelezwa bila kukwama. Wafanyabiashara hao wana uwezo wa kuhakikisha wanatafuta rasilimali ya madini ya mchanga ili kuweza kunusuru rasilimali ya mchanga iliyopungua Zanzibar.

Wanazuoni husema changamoto ni sehemu ya kupata fursa tusisubiri mpaka fursa hiyo iende kwa wengine na sisi tupo. Uhaba wa mchanga visiwani Zanzibar ulitazamiwa toka mwaka 2017 aliposema Waziri wa Kilimo Maliasili Mifugo na Uvuvi wakati huo Hamad Rashid Mohammed na sasa imerudiwa kusemwa na Rais Dkt. Shein, nadhani sasa ni utekelezaji ambao utaokoa mazingira husika. 

Rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini, Nelson Mandela alishawahi kusema “Mara zote huonekana haliwezekani mpaka lifanikiwe”, maneno haya yanawakumbusha Wafanyabiashara wanatakiwa kutambua fursa hii na kuifanyia kazi ipasavyo na kupata majibu kuwa kuna uwezekano wao kufanya biashara hii au la? 

Tanzania Zanzibar inajumla ya wakazi wapatao 900,000 kwa kisiwa cha Unguja huku Pemba wakiwa 400,000 na kufanya jumla ya wakazi Milioni 1.3, Ama hakika ni idadi yenye uhitaji mkubwa wa rasilimali ya madini ya Mchanga.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: