Mrembo wa Redd's Miss Tanzania 2014, Sitti Abbas Mtemvu akiwa katika picha ya pamoja na Mshindi wa pili,Lillian Kamazima (kulia) na Mshindi wa Tatu, Jihhan Dimachk mara baada ya kutawazwa rasmi usiku huu kwenye ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.

Na Mwandishi Wetu.

Kwa siku kumi, Kamati ya Miss Tanzania, Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo na Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) wameshindwa kutatua kitendawili cha kashfa ya Miss Tanzania 2014, Sitti Mtemvu.

Pande hizo zimeshindwa kutoa uamuzi kuhusu hatima ya Sitti Mtemvu katika medani hiyo ya urembo.

Kutwa nzima jana, Basata na kamati hiyo kupitia Kampuni ya Lino International Agency, waratibu wa Miss Tanzania walikutana makao makuu ya baraza kwa majadiliano kuhusu hatima ya mrembo huyo anayedaiwa kuongopa kuhusu umri wake na hivyo kukosa vigezo vya kumiliki taji hilo.

Kikao hicho kilichofanyika kwa takribani siku nzima, kililenga kufikia hatima ya mgogoro huo unaohusu umri sahihi wa mrembo huyo baada ya baraza hilo kufanya uchunguzi wao wa siku kumi, uliokamilika jana, Oktoba 30.

Ofisa habari wa baraza hilo, Agnes Kimwaga alisema ni kweli jana kilifanyika kikao kirefu katika ofisi hizo na kwamba msemaji mkuu wa suala hilo ni katibu mtendaji.

“Hili ni suala nyeti na msemaji mkuu ni katibu mtendaji wa Basata, Godfrey Mungereza na hakuna yeyote mwenye mamlaka zaidi ya kulizungumzia suala hilo.”

Naye Mungereza alipotafutwa ili kuzungumzia kashfa hiyo, hakupatikana na hata simu yake ya kiganjani haikuita.

Mkurugenzi wa Lino International Agency, Hashim Lundenga aliliambia gazeti hili jana kuwa ni mapema mno kuzungumzia suala hilo, kwani lipo chini ya baraza na wao kama waandaaji walifuata kanuni za mashindano na hivyo waliona Sitti alikuwa na uhalali wa kushinda taji hilo.

“Sisi kama waandaji tuliangalia cheti chake cha kuzaliwa alichokiwasilisha kwetu, masuala mengine yaliyoibuka baadaye yapo chini ya Basata na wao ndio wazungumzaji wakuu, tusubiri watoe tamko lao.

Mimi kama Lundenga siwezi zungumza chochote na vyombo vya habari wala Sitti mwenyewe.” Nyaraka zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha kuwa Sitti alizaliwa Mei 31, 1989 na siyo Mei 31, 1991 kama ilivyoelezwa na Kamati ya Miss Tanzania.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: