SIKU moja baada ya serikali kufunga Hospitali ya Chuo cha Kimataifa cha Matibabu na Teknolojia (IMTU), kwa madai ya kuendeshwa kwa kukiuka taratibu za tiba, hatua hiyo imefikiwa ili kukinusuru chuo hicho na adhabu ya utupaji viungo vya binadamu.

Kwamba uamuzi huo umefikiwa kutuliza hasira za makundi mbalimbali, kikiwamo Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), waliolaani utupaji huo.

Wakati hatua hiyo ikionekana kutaka kunusuru kufungwa kwa chuo, viongozi wa serikali ya wanafunzi chuoni hapo wamesema kikifungwa watakuwa wanaonewa kwakuwa wanaostahili adhabu ni utawala.

Chanzo hicho kimesema kama chuo hicho kingefungwa, ingeathiri wanafunzi wengi ambao wengine wanasubiri kufanya mitihani yao ya mwisho kumaliza elimu yao ya tiba.

Kitendo cha Manispaa ya Kinondoni kufanya ukaguzi huku timu za uchunguzi wa suala hilo zikiwa kazini, kinalenga kutoa ahueni kwa chuo kuendelea na shughuli zake.

Itakumbukwa kuwa serikali iliunda tume ya watu 15 kuchunguza jambo hilo, huku nalo Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam likiteua timu ya kufuatilia watuhumiwa waliohusika na utupaji viungo hivyo.

Imebainika kuwa ufungaji hospitali hiyo unaonekana uliratibiwa mapema kwakuwa wakati timu ya wakaguzi hao ikifika hospitalini hapo, hakukuwa na mgonjwa aliyelazwa tofauti na ilivyo kawaida.

Baadhi ya wafanyakazi walidokeza kuwa adhabu ya kufungwa kwa hospitali hiyo inaweza kukinusuru chuo kwakuwa ripoti itakayotolewa na tume ya watu 15 iliyoundwa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, inaweza kutoa pendekezo la aina hiyo.

“Adhabu hii ya kufunga hospitali ni kama kinga ya kuunusuru uongozi wa chuo hicho ambao kimsingi na kisheria ndio wanaostahili kufanya kazi za utafutaji, usafirishaji, utunzaji, uhifadhi na kuzika au kuchoma miili hiyo kwa kufuata miiko ya kazi hiyo inavyotaka,” kilisema chanzo hicho.

Juzi timu ya Menejimenti ya Afya ya Manispaa ya Kinondoni, iliyokuwa imeongozana na Mganga Mkuu wa Manispaa, Dk. Gunini Kamba, wameifunga hospitali hiyo baada ya kubaini kuwepo kwa upungufu sehemu mbalimbali.

Alisema upungufu walioubaini ni kutokuwa na wauguzi, vifaa vya kutosha, sehemu ya kuteketeza taka ngumu, wamekuwa wakichanganya dawa zilizokwisha muda na ambazo zinatumika katika kabati moja.

Dk. Gunini alisema: “Upungufu wa madaktari umesababisha tumkute mfanyakazi mmoja wa msalaba mwekundu akifanya kazi za madaktari.”

Alisema kuwa kama viongozi wa IMTU watataka kuendelea na huduma ya hospitali, wanatakiwa kurekebisha matatizo hayo waliyoambiwa ikiwamo kutuma maombi upya kwa kuanzia manispaa.

Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa IMTU, Meekson Mambo, alisema tangu sakata hilo lianze, limesababisha wanafunzi kushindwa kusoma kwa uhuru na muda mwingi kuutumia katika kutafakari hatima yao.

Mambo, alisema wanapinga vikali kauli ya Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk. Primus Saidia ya kutaka serikali ikifute chuo hicho.

Rais huyo alisema kuwa kiongozi wa MAT, alitoa kauli hiyo bila kutafakari kwa kina mustakabali wa uamuzi anaotaka uchukuliwe, kwani hatua hiyo ni sawa na kutaka kuwahukumu wanafunzi wasiohusika na tukio hilo.

Alifafanua kuwa alitarajia Dk. Saidia, angesikiliza maoni ya wanafunzi juu ya tukio hilo na kuwaona viongozi na mmiliki wa chuo kupata ukweli.

Aliongeza kuwa uamuzi wowote utakaofanywa kukifuta chuo hicho utakuwa na athari kubwa kwa wanafunzi, na hawatakubali hatua hiyo.

“Tumeshawaambia watu wanaofanya uchunguzi kuwa hatutakubali wazo la kufutwa kwa chuo au kufungwa… sisi tuna kosa gani, kina nani walitupa viungo?” alihoji.

Waziri Mkuu wa Serikali hiyo, Edward Mhina, alisema jumuiya yao inalaani kitendo cha utupaji wa miili hiyo kwa kuwa inakiuka maadili na sheria za mafunzo ya udaktari.

“Tanzania ina uhaba wa madaktari, MAT inashinikiza chuo hiki kifutwe, tunaelekea wapi? Tuache vyombo vya dola vifanye kazi yake,” alisema.

Mabaki ya miili ya binadamu yaliyokuwa kwenye mifuko 85 ya plastiki, yalikutwa wiki iliyopita yakiwa yametelekezwa maeneo ya Mto Mpiji, Mbweni nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam na haikujulikana mara moja imetoka wapi, kabla ya polisi kufanya uchunguzi.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: