Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.

Bunge la Bajeti la mwaka wa fedha wa 2014/15 linatarajia kufanya vikao vyake hadi saa mbili usiku pamoja na siku za Jumamosi ikiwa ni moja ya njia za kufidia siku 28 zilizopunguzwa kufanya vikao hivyo.

Tofauti na Bunge la Bajeti lililopita ambalo lilifanya vikao kwa siku 80, mwaka huu litafanya vikao vyake kwa siku 52 kuanzia Mei 6 hadi Juni 27, mwaka huu.

Mabadiliko hayo yametokana na kuliwa kwa baadhi ya siku na Bunge Maalumu la Katiba lililoahirisha vikao vyake Ijumaa iliyopita hadi Agosti mwaka huu.

Kutokana na uchache huo wa siku, Bunge linatarajiwa kupitisha mapendekezo ya kuongeza dakika 65 zaidi ya muda uliopangwa kwa mujibu wa Kanuni za Bunge za mwaka 2013, pia vikao kufanyika hadi Jumamosi.

Kwa mujibu wa Kanuni ya 28, vikao vya Bunge hutakiwa kuanza saa tatu asubuhi hadi saa saba mchana kwa Jumatatu hadi Ijumaa na kuahirishwa hadi saa 11:00 jioni ambako huendelea hadi saa 1:45 jioni.

Katika mapendekezo mapya, Bunge linakusudia kuanza vikao saa 3:00 asubuhi hadi saa 7:00 mchana na kurudi saa 10:00 jioni hadi saa mbili usiku.

Taarifa iliyotolewa juzi na Idara ya Habari, Elimu kwa Umma na Uhusiano wa Kimataifa ya Ofisi ya Bunge ilisema siku za Ijumaa Bunge litaahirisha vikao vyake vya mchana saa moja kabla ya muda wa kawaida wa saa 7:00.

Iwapo Bunge litapitisha mapendekezo hayo, kutakuwa na ongezeko la saa sita na nusu kila wiki, hatua ambayo inaweza ikaongeza kidogo muda wa kujadili masuala mbalimbali ya Bajeti ya Serikali.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: