Shirika la Kimataifa la Mtandao wa Ulaya wa Madeni na Maendeleo, European Network on Debt and Development (Eurodad) watafanya ziara ya kiuchunguzi kuhusu masuala ya uwazi katika kodi katika nchi za Ulaya kuanzia tarehe 20 Oktoba mpaka tarehe 5 Novemba mwaka 2013. Uchunguzi huo utaendeshwa na wataalamu waliobobea wa masuala ya kodi na maendeleo. Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali wa Bunge la Tanzania Zitto Zuberi Kabwe ameteuliwa kuongoza Jopo la uchunguzi huo.
Eurodad ni Mtandao wa Mashirika yasiyo ya kiserikali yapatayo 48 kutoka nchi 19 za Ulaya ambayo yanajihusisha na masuala ya kufutia madeni nchi zilizoendelea, misaada yenye maana na kodi za haki. Mashirika haya yamekuwa kwenye kampeni ya kupinga utoroshwaji wa fedha kupitia ukwepaji kodi unaofanywa na mashirika ya kimataifa kwa nchi zinazoendelea. Zitto amekuwa mmoja wa wabunge wanaosimamia hoja ya kutaka Watanzania waliotorosha fedha kwenda nje warejeshe na kufunguliwa mashtaka.
Mwaka 2012 aliwasilisha hoja binafsi Bungeni na kupitishwa kuwa Azimio la Bunge ya kutaka uchunguzi kuhusu utoroshwaji wa fedha na kufichwa nje kama Uswiss. Kikosi Kazi cha Serikali kutekeleza Azimio hilo la Bunge kinatarajia kuwasilisha taarifa yake katika Mkutano wa Kumi na Sita wa Bunge. Siku ya Jumatatu tarehe 21 Oktoba Zitto atakutana na Waziri wa Fedha wa Uswiss na maafisa wa mabenki na asasi zisizo za kiserikali zilizopo jijini Geneva. Pia Zitto atahudhuria mkutano wa Kamati ya Kodi ya Umoja wa Mataifa katika kampeni ya kubadili mfumo wa kodi za kimataifa ili kuzuia unyonyaji wa nchi za Kiafrika unaofanywa na Makampuni makubwa ya Kimataifa.
Baada ya Geneva Zitto atatembelea nchi za Luxembourg na Brussels kabla ya kwenda Norway ambapo atamalizia ziara yake kwa Jopo la Wataalamu wa masuala ya kodi na Maendeleo kuandika taarifa maalumu yenye mapendekezo kuhusu kuzuia utoroshaji wa fedha kutoka Afrika.
Zitto atakwenda jijini London kutoa mada kuhusu masuala ya kodi za kimataifa katika mkutano wa Uwazi (Open Government Partnership). Mwenyekiti wa PAC Tanzania atafanya mazungumzo na Mwenyekiti wa PAC Uingereza Bi Margaret Eve Hodge, Lady Hodge MBE, PC, MP kuhusu masuala mbalimbali ya ushirikiano wa mabunge mawili na kuendeleza wito wake kwa makampuni ya kimataifa kulipa kodi zao barani Afrika na kuacha tabia ya kutumia ‘Tax Havens’ kukwepa kodi na kufukarisha nchi za Kiafrika.
Toa Maoni Yako:
0 comments: