Rahim Kangezi akifafanua jambo kuhusiana na mapato na matumizi ya klabu hiyo, kushoto ni Ibrahim Salim ambaye ni meneja wa fedha wa timu hiyo.
---
Na Mwandishi Wetu
TIMU ya soka ya African Lyon ya jijini Dar es Salaam imetangaza hasara ya sh. milioni 180.3 kutokana na ushiriki wake katika msimu uliopita wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Lyon ni miongoni mwa timu tatu zilizoshuka daraja kutoka katuika ligi hiyo kubwa ya soka nchini, nyingine ni Toto African na Polisi Moro.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam, Meneja wa Fedha wa Lyon, Ibrahim Salim, alisema timu yao imetumia zaidi ya sh. 388,614,500 kwa ajili ya maandalizi hadi michezo yake.
Salim alisema katika makusanya na matumizi yao, walilazimika kutumia kiasi cha sh. milioni 268.09 katika mzunguko wa kwanza, kabla ya kutumia sh. 123.6.
"Katika matumizi yote haya, fedha ambayo tumeiingiza kama klabu kupitia viingilio na vyanzo vingine ni sh. milioni 207.6, na hapo ndipo unapopata tofauti ya sh. milioni 180.3, ambayo ni hasara," alisema Salim.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Lyon, Rahim Kangezi, alisema soka ya Tanzania inaendeshwa kwa hasara huku wenye dhamana ya kusaidia wakiwa hawatendi haki kwa baadhi ya vipengele.
Kangezi alisema timu yake imeingia katika hasara ya sh. milioni 180.3 kutokana na uendeshaji, lakini bado wameshuka daraja, huku akisisitiza kuwa hakuna anayeshutumiwa kwa kushuka kwa timu hiyo.
"Unaweza kuona changamoto ambayo tunakumbana nayo katika uendeshaji wa taasisi kamam a hizi, tunapopiga kelele kwa wadhamini kutuwahishia fedha tunamaanisha.
"Angalieni mfano mdogo kwa fedha za wadhamini (Vodacom), ambazo awamu ya mwisho zimetufikia Mei mwaka huu, tukiwa tumebakiza mechi moja ya Ligi Kuu, sasa zingetusaidia katika nini? Alihoji mmiliki huyo.
Akizungumzia kuhusu uendeshwaji wa Ligi Kuu na changamoto walizokutana nazo, Kangezi alisema bado hakujakuwa na usimamizi mzuri katika kuhakikisha kuwa ligi hiyo inakuwa bora.
Katika hatua nyingine, Kangezi alisema timu yake inajivunia mafanikio waliyochangia kusogeza maendeleo ya soka nchini kutokana na kutoa nafasi kwa Mrisho Ngassa kwenda kujaribu soka ya kulipwa na kucheza katika kikosi cha Seattke Soundowns dhidi ya Manchester United.
"Tulifanikiwa pia kuileta timu kubwa ya Ligi Kuu ya Brazil (Atletico Parenese) kwa ziara ya kimichezo nchini, tulitoa wachezaji watano kwa ajili ya kujaribu soka ya kulipwa sambamba na kufanya semina mbili juu ya uongozi wa michezo," aliongeza.
Toa Maoni Yako:
0 comments: