Rais wa Chama cha Wakala wa Forodha na Uondoshaji wa
Shehena Tanzania (TAFFA) Bw. Stephen Ngatunga wakati akitoa ufafanuzi
kuhusu mkutano wa Kimataifa wa Wakala wa Forodha katika nchi za Afrika
na Mashariki ya kati (RAME 2013) utakaofanyika jijini Dar es salaam
kuanzia Juni 19. Kushoto ni Mkurugenzi mshauri wa TAFFA.
Imeelezwa kuwa Tanzania itanufaika zaidi kibiashara kupitia bandari
ya Dar es salaam, Mtwara na Tanga kutokana na serikali kuamua kufanya
maboresho makubwa katika sekta ya usafiri wa Bandari na reli.
Hayo
yamebainishwa leo jijini Dar es salaam na Rais wa Chama cha Wakala wa
Forodha na Uondoshaji wa Shehena Tanzania (TAFFA) Bw. Stephen Ngatunga
wakati akitoa ufafanuzi kuhusu mkutano wa Kimataifa wa Wakala wa
Forodha katika nchi za Afrika na Mashariki ya kati (RAME 2013)
utakaofanyika jijini Dar es salaam kuanzia Juni 19.
Amesema
Tanzania kupitia Chama cha Wakala wa Forodha na Uondoshaji Shehena
Tanzania (TAFFA) itakuwa mwenyeji wa mkutano huo utakaowashirikisha
mawakala 300 wa makampuni ya usafirishaji na upokeaji wa mizigo ,
wafanyabiashara, maafisa wa serikali na mabalozi mbalimbali kutoka nchi
za Mashariki ya kati.
Rais wa Chama cha Wakala wa Forodha na Uondoshaji wa
Shehena Tanzania (TAFFA) Bw. Stephen Ngatunga akisisitiza kuhusu
serikali kulifanyia kazi suala uundaji wa mkakati wa kutangaza bandari
zetu nje ya nchi kwa kufungua ofisi katika nchi zinazotuzunguka kwa
lengo la kuongeza watumiaji wa bandari . Kushoto ni Mkurugenzi mshauri
wa TAFFA na Bw. Jimmy Mwalugerwa (Mkurugenzi TAFFA).
Amesema mkutano huo wa siku 3 utakuwa na manufaa makubwa kwa
wafanyabishara kutoka Tanzania kujenga mahusiano na kunufaika na fursa
mbalimbali zilizo katika eneo zima la Afrika na Mashariki ya kati
,kuitangaza Bandari ya Dar es salaam, Tanga na Mtwara pamoja na kukuza
utalii nchini.
Amefafanua kuwa Tanzania kupitia TAFFA
inakuwa mwenyeji wa mkutano huo kutokana na pendekezo lililopitishwa
katika mkutano mkuu wa dunia wa mwaka 2012 uliofanyika mjini Los
Angeles, Marekani.
Ameongeza kuwa katika mkutano huo
wa Juni 19, rais wa Shirikisho la Kimataifa la Wakala wa Forodha na
Uondoshaji wa Shehena (FIATA) Bw. Stanley Lim pamoja na wajumbe
waandamizi wa shirikisho hilo kutoka nchi wanazoziwakilisha watajadili
mambo mbalimbali ya kuboresha biashara katika ukanda wa nchi za Afrika
na Mashariki ya Kati (RAME).
Viongozi wa Chama cha Wakala wa Forodha na Uondoshaji wa Shehena Tanzania (TAFFA). Picha/Habari na Aron Msigwa – MAELEZO.
Katika hatua nyingine Bw. Ngatunga amefafanua kuwa maboresho
yanayoendelea hususan katika bandari ya Dar es salaam yanaifanya
Tanzania kuwa katika nafasi nzuri ya kupanua wigo wa kunufaika na
ongezeko la fursa za biashara kwa nchi zisizo na ukanda wa bahari
zikiwemo Burundi, Rwanda , Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Uganda,
Zambia na Malawi kuendelea kutumia usafiri wa reli na Bandari za
Tanzania kusafirisha mizigo.
Amesema kitendo cha
serikali kufanya maboresho makubwa ya kiutendaji katika bandari na reli
kimesaidia kuendelea kuleta imani kwa wafanyabishara kutoka nchi
mbalimbali zisizo za ukanda wa Bahari kupitisha mizigo yao na kuongeza
kuwa matatizo mbalimbali yaliyokuwa yakikwamisha uondoshaji wa shehena
bandarini yamefanyiwa kazi.
Ameeleza kuwa serikali
kukubali kulifanyia kazi suala la ukusanyaji wa mapato ya Bandari na
kuagiza lifanyike kupitia benki badala ya utaratibu wa awali wa kulipa
fedha moja kwa moja bandarini limepunguza urasimu na kuongeza
uwajibikaji na ukusanyaji wa mapato katika sekta hiyo.
“Kwanza suala la ukusanyaji wa mapato bandarini lilisababisha usumbufu mkubwa, waziri wa uchukuzi alivyoingia tulimweleza na tukamwomba alifanyie kazi na jambo hilo likatekelezwa sambamba na uboreshaji wa huduma za usafiri wa reli ili kupunguza mrundikano wa makontena bandarini kanma ilivyoainishwa katika bajeti ya uchukuzi ya 2013/2014 limetufariji sana” ameeleza Bw.Ngatunga.
Aidha ameiomba serikali kulifanyia kazi suala uundaji wa mkakati wa kutangaza bandari zetu nje ya nchi kwa kufungua ofisi katika nchi zinazotuzunguka kwa lengo la kuongeza watumiaji wa bandari na kukabiliana na ushindani pamoja na kuwachulia hatua za kisheria wale wote watakaokwamisha ufanisi wa shughuli za bandari nchini.
Toa Maoni Yako:
0 comments: