SIKU chache baada ya Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kuwakamata askari 16 wakituhumiwa kujihusisha na biashara ya magendo, askari wengine wawili wa jeshi hilo wamekamatwa mkoani Kilimanjaro wakiwa na shehena kubwa ya bangi wakiisafrisha kwenda nchini Kenya.

Askari hao walikamatwa Mei 19 mwaka huu saa nne usiku eneo la Kilemapofu, Wilaya ya Moshi Vijijini wakiwa na magunia 18 ya bangi ambayo walikuwa wameyapakia kwenye gari la Mkuu wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) mkoani Arusha aina ya Toyota Land Cruiser lenye namba PT 2025.

Akithibitisha kukamatwa kwa askari hao, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz (PICHANI) alisema askari hao walikuwa wakipeleka bangi hiyo Wilaya ya Rombo kwa mfanyabiashra mmoja ambaye hakutaka kumtaja jina lake.

Kamanda Boaz aliwataja askari waliokamatwa na wanashikiliwa kwenye kituo kikuu cha polisi katika mji mdogo wa Himo kuwa ni F.1734 Koplo Edward (dereva) wa kikosi cha kutuliza ghasia (FFU) mkoani Arusha na G.2434 Konstebo George wa kituo cha polisi Ngarenanyuki Wilaya ya Arumeru.

Alibainisha kuwa kukamatwa kwa askari hao kunatokana na operesheni ya kukabiliana na dawa za kulevya inayofanywa na polisi katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro.

Alisema operesheni hiyo imefanyika kikamilifu katika Mkoa wa Arusha uliokuwa ukitumika kupitishia bidhaa hiyo, na sasa wahusika wameamua kuutumia Mkoa wa Kilimanjaro.

“Baada ya kuwahoji askari wale, walidai kuwa walikodishwa na mfanyabiashara huyo kuipeleka bangi hiyo wilayani Rombo tayari kwa kusafirishwa kwenda nchini Kenya ambako inaaminika kuna soko kubwa,” alisema.

Kamanda Boaz alisema hivi sasa polisi wa Kilimanjaro kwa kushirikiana na wenzao wa Arusha wanafanya uchunguzi kubaini mtandao wa askari hao unaojihusisha na vitendo haramu.

Aliongeza kuwa hatua inayofuata kwa askari hao ni kufunguliwa mashtaka ya kijeshi na iwapo watakutwa na hatia watafukuzwa kazi kisha watafikishwa katika mahakama za kiraia.

Kamanda Boaz alibainisha kuwa kwa kawaida askari wanapotoka mkoa mmoja kwenda mwingine hupatiwa kibali maalumu cha kusafiria (Movement Order). Alisema kibali hicho husaini kila mkoa ambao askari husika hupita, lakini waliokamatwa na bangi hawakuwa nacho.

Kamanda Boaz alibanisha kuwa kwa hali ilivyo askari hao waliondoka na gari la mkuu wa FFU bila kumpa taarifa wala kupata kibali chake.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: