Mwaka huu umeanza na ingizo jipya kwenye tasnia ya muziki hpa nchini baada ya mwanadada Vanessa Mdee kutoa wimbo wake mpya unaofahamika kama Closer.
Mwanadada huyu, ambaye alishirikiana na Ommy Dimpoz kwenye wimbo wake wa Me and You mwishoni mwa mwaka jana, amewashangaza wengi kwa kipaji alichokionyesha katika wimbo wake wa Closer.
Vanessa ambaye ni mtangazaji wa kituo cha redio cha Choice FM lakini pia anafanya kazi na kituo cha luninga cha MTV, amejipatia umaarufu zaidi baada ya kuwa mtangazaji wa kipindi cha kusaka vipaji cha Epiq Bongo Star Search.
Wimbo huo ambao umetayarishwa na waandaji mahiri wa muziki nchini, Hermy B na Pancho Latino, unamfanya Vanessa kuwa mmoja wa waimbaji wa kike wanaorajiwa kufanya vizuri.
Hermy B na Pancho wanasifika kwa kufanya kazi na wanamuziki wakali kama AY, Chidi Benz na Nakaaya.
Wimbo wa Closer ulianza kuandaliwa miaka miwili iliyopita kabla ya Vanessa kuamua kuuachia rasmi wiki mbili zilizopita. Akiuzungumzia wimbo huo, Vanessa anasema ni mchanganyiko wa ‘Afro pop, RnB, Soul na Hip pop’.
Tokea wimbo huo umeachiwa rasmi wiki mbili zilizopita umeshika kwa kasi, kiasi ambacho wengi wanaamini ni mwanzo mzuri kwa mwanadada huyu.
Toa Maoni Yako:
0 comments: