Na Mohammed Mhina wa Jeshi la Polisi- zanzibar
Imeelezwa kuwa, kuanzia sasa Askari Polisi yeyote atakayefukuzwa kazi
ama kuachishwa kutokana na makosa ya kiutendaji atalipwa stahili zake
zote tofauti na zamani ambapo askari aliyekuwa akifukuzwa alikuwa
akitoka mikono mitupu.
Ufafanuzi
huo umetolewa na Mkuu wa Utawala na Rasilimali watu wa Jeshi la Polisi
Kanda ya Zanzibar Kamishna Msaidizi Mwandamizi Kenneth Kasseke, wakati
akizungumza kwenye mkutano wa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Mh. Perera
Juma Silima anayeitembelea Zanzibar.
Kamanda
Kasseke ametoa ufafanuzi huo alipotakiwa kujibu hoja mbalimbali
zilizoulizwa na askari wakati wa mkutano wa Mh. Silima uliowashirikisha
Askari na Maafisa wanadhimu wakiwemo Makamanda wa Polisi wa Mkoa mitatu
ya Zanzibar.
Kamanda
Kasseke amesema Jeshi la Polisi limefikia hatua hiyo baada ya kuona
kumekuwapo na malalamiko ya msingi kutoka kwa baadhi ya askari kuwa
wamekuwa wakifukuzwa kazi bila ya kulipwa haki zao hata baada ya kukatwa
fedha kuchangia kwenye mifuko mbalimbali ya hifadhi za jamii.
Kutokana
na hali hiyo Kamanda Kasseke amesema imeonekana kuwa sio busara wala
haki kwa askari huyo kunyimwa fedha hizo ambazo zinatokana na makato
kwenye sehemu ya mishahara yao ambayo kama isingekatwa angekuwa amepewa
ama kujiwekea mwenyewe akiba benki.
“Fedha
hizo ni sawa na mtumishi aliyejiwekea akiba na kwamba zingeweza
kumsaidia wakati wowote akiwa kazini ama hata baada ya kumaliza muda
wake wa utumishi Jeshini”. Alisema Kamanda Kasseke huku akishangiliwa na
Askari waliohudhuria katika mkutano huo.
Kamanda
Kasseke alitakiwa na Mh. Silima kujibu hoja mbalimbali zilizoulizwa na
askari ikiwemo la kutokulipwa fedha zao baada ya kufukuzwa kazi na hata
kufikishwa mahakamani kutokana na makosa mbalimbali yakiwemo ya bahati
mbaya hata baada ya kulitumikia Taifa kwa muda mrefu.
Na
kwa upande wake Waziri Silima akizungumza kwenye mkutano huo, amesema
kuwa pamoja na juhudi zinazochukuliwa na serikali za kuboresha makazi ya
askari ikiwa ni pamoja na nyumba mpya za Askari katika
maeneo mbalimbali hapa nchini, lakini bado hali ya majengo mengi
wanayoishi askari Polisi makambini yana hali mbaya.
Amesema amelazimika kufanya ziara ili kujionea mwenyewe hali hiyo badala ya kusikia kutoka kwa baadhi ya Maafisa na askari.
Katika
mkutano huo ambao uliendeshwa kwa kuanza kupokea hoja, maoni, kero na
maswali mbalimbali kutoka kwa Askari Polisi wa Vikosi mbalimbali, Waziri
Silima pia alifurahishwa na hoja za msingi zilizotolewa na askari hao
na kusema kuwa zikipatiwa ufumbuzi malalamiko kama hayo yatapungua.
Lakini
pia Waziri Silima alipongeza hatua mbalimbali zilizochukuliwa na
zinazoendelea kuchukuliwa na uongozi wa juu wa Jeshi la Polisi hapa
nchini akiwemo Mkuu wa Jeshi la Polisi Inspekta Jenerali saidi Mwema
katika kutekeleza baadhi ya mambo wenye lengo la kuboresha ustawi wa
kila askari Polisi.
Pamoja
na kukemea vitendo vya kudai na kupokea rushwa vinavyofanywa na baadhi
ya askari wakiwemo wa Kikosi cha Usalama barabarani, lakini Waziri
Silima pia amewahakikishia askari Polisi kote nchini kuwa Serikali
itafanya kila liwezekanalo ili kuona kila askari Polisi ananufaika na
kazi anayoifanya.
Ametoa
wito pia kwa wananchi kuendelea kushiirikiana na Jeshi la Polisi kwa
kutoa taarifa za siri zitakazowezesha kukamatwa kwa wahalifu mbalimbali
na kuwafanya waishi kwa usalama na amani.
Amesema
Serikali haifurahii kuona kila kukicha kuna mwananchi aliyefanyiwa
vitendo vya kihalifu kama vile mauaji, unyang’anyi wa kutumia silaha ama
kusambaziwa dawa za kulevya na watu wanaofahamika na bila ya
kuchukuliwa hatua.
“Tunaendelea
kuwaomba sana wananchi washirikiane na sisi kwa kutupatia taarifa ili
tuzishughulikie”. Ndivyo alivyomaliza Waziri Silima.
Toa Maoni Yako:
0 comments: