Meneja wa Kitengo cha Habari na Ushauri, HakiElimu, Nyanda
Shuli (kushoto) akijibu maswali anuai ya wanahabari katika mkutano
huo..
Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu,
Bi. Elizabeth Missokia (kulia) akitoa tamko kwa wanahabari kuhusiana
na mgomo mchana huu jijini Dar es Salaam. Wa pili kutoka kulia ni
Meneja wa Kitengo cha Habari na Ushauri, HakiE.
---
Na Joachim Mushi, Thehabari.com
TAASISI ya HakiElimu nchini imeishauri
Serikali pamoja na Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) kufikia
makubaliano haraka iwezekanavyo, ili kumaliza mgomo uliopo kwani
waathirika zaidi na mgomo huo si wao bali ni ni wanafunzi.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es
Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu, Bi. Elizabeth Missokia
alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusiana
na mgomo wa walimu unaoendelea maeneo mbalimbali nchini.
Alisema kila mwanafunzi ana haki ya
kujifunza na kuelimishwa, kitu ambacho hawakipati kwa sasa kutokana
na mgomo wa walimu wanaoshinikiza Serikali iwaongeze mishahara pamoja
na kuwaboreshea mazingira ya kazi zao.
Mkurugenzi huyo alisema kauli ya
Serikali kudai haina uwezo wa kuboresha maslahi na mazingira ya kazi
ya watumishi wake haileti unafuu wa maisha kwa watumishi wa
umma hivyo kushauri iangalie namna ya kufanya kumaliza mgogoro huo.
“HakiElimu inasisitiza kwamba nchi
itafanikiwa kuboresha elimu endapo tu itawekeza kwa walimu kwa
kuboresha mazingira ya kazi, maslahi ya walimu, kuwashirikisha walimu
katika maamuzi kuhusu masuala ya elimu na kuwapa walimu mafunzo
kazini. Elimu bora haiwezi kuletwa na walimu walio hoi,” alisema
Missokia.
Aidha amewataka walimu kuhakikisha
wanadai haki zao huku wakiendelea kuwajibika kwa kufundisha na
kuendeleza elimu yetu, kwani wanamgogoro na Serikali na wala si
wanafunzi na jamii kwa ujumla.
“HakiElimu inawakumbusha walimu
kuwajibika. Wadai haki zao, huku wakitimiza wajibu wao wa kufundisha
na kuendeleza elimu yetu. Wafundishe kwa bidii bila kinyongo, kwa
kuwa wasipowajibika watakuwa wanawaumiza wanafunzi na jamii kwa
ujumla. Mgogoro uliopo ni baina yao na Serikali, na si wanafunzi,”
alisema Mkurugenzi huyo Mtendaji.
“Viongozi wa Serikali wasiwabeze walimu; kwa kufanya hivyo wanawakatisha tamaa. Hata kama baadhi ya walimu hawakusoma kwa miaka mingi kama ilivyo kwa fani nyingine, wana umuhimu mkubwa sana. Ndio wanaowaandaa watanzania wa leo na kesho kimtazamo na kimaarifa. Hivyo, kudai kuboreshewa mazingira ya kazi ni haki yao; na Serikali inaweza kutimiza wajibu wake kwa kuwasikiliza na kushauriana nao bila ubabe na kejeli,” alisema.
Pamoja na hayo ameliomba Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuingilia kati mgogoro huo na kutenga
muda kujadili suala hilo kwa kina ikiwa ni pamoja na kuishauri
serikali, hasa kuhusu tahadhari za kuchukua ili tatizo kama hili
lisitokee tena.
“Bunge lina wajibu wa kuishauri na
kuisimamia Serikali kuhusu sera, utendaji na usimamizi wa elimu
nchini. Inasikitisha kwamba Bunge linakwepa kujadili tatizo hili kwa
maelezo kwamba liko mahakamani. Tunaamini kwamba mahakama
italiangalia suala hili na kutenda haki, lakini wajibu wa Bunge uko
pale pale…” alisema Bi. Missokia.
Amekiri kwamba ni kweli gharama za
maisha zinazidi kupanda, huku mfumuko wa bei nao unaendelea kuwaumiza
watumishi kila siku, hivyo kuishauri Serikali kutafuta vyanzo mbadala
vya mapato ili kuweza kuwaboreshea mapato watumishi wake.
“Serikali ijijengee utaratibu wa
kuboresha mazingira ya watumishi wake, na si kusubiri kwenda
mahakamani kuzuia watumishi kugoma. Watumishi wa umma watafanya kazi
kwa ari endapo tu wameridhika na mazingira ya kazi na maslahi yao; na
si kwa kutumia uamuzi wa mahakama peke yake.”
Toa Maoni Yako:
0 comments: