Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania(KKKT) na  Mhadhili, Mradi wa Chuo Kikuu cha Amani Njombe, Tanzania Mch. Dr. Elia Shabani Mligo (kushoto) akiwaonyesha waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam kitabu chake alichoandika kitakachomsaidia mwanafunzi kuandaa kuandika utafiti kwa urahisi kwa kutumia lugha ya kiswahili. Kulia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya EGYS ambaye ni mchapishaji Mkumbo Mitula.
---
Ndugu zangu Waandishi wa habari, Wanataaluma mbalimbali katika Vyuo Vikuu na  Watanzania wenzangu wote. Mimi ni Mch.Dk.Elia Shabani Mligo  mtumishi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania  Dayosisi ya Kusini Njombe. Mimi ndiye mwandishi wa Kitabu kipya cha Utafiti kwa Lugha ya Kiswahili kiitwacho: JIFUNZE UTAFITI: Mwongozo kuhusu Utafiti na Uandishi wa Ripoti yenye Mantiki  kilichotolewa na Ecumenical Gathering, na kuchapishwa na Jamana Printers Dar esa laam.  Mimi ninatoka Mkoa mpya wa Njombe, Wilaya mpya ya Wanging’ombe, na ni mwalimu katika mradi mpya wa Chuo Kikuu cha Amani ambao unamilikiwa na KKKT Dayosisi ya Kusini na kuendeshwa chini ya Chuo Kikuu Kishiriki cha Iringa.

Katika hadhara hii, nataka kujibu swali moja muhimu: Je, ni kwa nini nimeandika kitabu hiki cha Kiswahili ili kitumike kufundishia utafiti katika Elimu ya Juu wakati vyuo vingi hufundisha taaluma kwa lugha ya Kiingereza? Kwa mtazamo wa juu juu mtu yeyote anaweza kuona kuwa hakukuwa na umaana wowote wa kuandika kitabu hiki katika lugha isiyotumika kufundishia. Katika kujibu swali la hapo juu, nitaanza kwanza kwa kueleza uzoefu wangu mimi mwenyewe kuhusu matumizi ya lugha za kigeni kufanya utafiti, na uzoefu wangu wa kuona jinsi lugha hizi za kigeni zikitumika katika Elimu ya Juu.

Nilipojiunga na Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira kwa ajili ya Shahada ya kwanza katika Theologia mwaka 1995 kila mwanafunzi miongoni mwetu alitakiwa kuandika maandiko kama sehemu ya madai kwa ajili ya kuhitimu. Ilituwia vigumu sana kwa wanafunzi tulio wengi kuuelewa utafiti ni kitu gani kwa sababu tulikuwa wageni na msamiati huo. Hatukufanya utafiti tukiwa Sekondari.

Utafiti ilikuwa ni jambo letu la kwanza kabisa. Ugumu tuliouona kwa sehemu kubwa ulisababishwa na lugha iliyotumika. Lugha ya Kiingereza haikuwa yetu ilikuwa ni lugha ambayo ni ya kufundishia tu siyo kwa ajili kazi yetu halisi. Tulifundishwa utafiti kwa lugha ya Kiingereza, lakini utafiti wenyewe tuliufanya kwa lugha ya Kiswahili kwa sababu tulilazimika kwenda kufanya utafiti kwenye maeneo ambako watu hawakuijua lugha ya Kiingereza. Baada ya kurudi kutoka kwenye utafiti tulilazimika kubadili Kiswahili kwenda Kiingereza, lugha ambayo tuliitumia katika kuandika ripoti zetu za utafiti.

Mch. Dr. Elia Shabani Mligo akifanya mahojiano na mwandishi wa habari.
Jambo hili la kubadili badili lugha lilifanya utafiti tulioufanya usiakisi hasa yale tuliyoyapokea kutoka kwa watoa habari maana kubadili kutoka lugha moja kwenda nyingine kulipunguza maana halisi ya yale tuliyoyapata. Hivyo, katika mchakato huo, niligundua wazi kuwa Lugha ya Kiswahili ilihitajika siyo tu katika kufanya utafiti, bali hata katika kujifunza utafiti wenyewe. Nilianza kuona kuwa mtafiti akiuelewa utafiti kwa lugha yake na kwa misamiati ambayo ameizoea tangu utoto wake, ataufanya kwa utasaha maana atakuwa anauelewa vizuri.

Jambo la pili linahusu hali halisi ya uwezo wetu sisi Watanzania katika kutumia Lugha ya Kiingereza katika Elimu ya Juu. Nilipoitwa kujiunga na masomo ya Shahada ya Uzamili katika Chuo Kikuu cha Oslo pale nchini Norway, niliwakuta Waafrica mwenzangu wengine watatu na Mzungu mmoja Mnorway. Jumla tulikuwa wanafunzi watano. Waafrika wengine walitoka Kenya, Zimbabwe, na Ghana. Katika mawasiliano ya Kiingereza yaliyokuwa yakifanyika darasani au mahali pengine popote mimi Mtanzania nilionekana kuwa sijiwezi kwa sehemu kubwa kujieleza kwa lugha ya Kiingerza kuliko wenzangu wa mataifa haya niliyoyataja.

Hata hivyo, hii haikumaanisha kuwa sikuijua taaluma niliyoitwa kuisome, la hasha. Shida ilikuwa ni lugha. Lugha ya Kiingereza haikuwa sehemu ya utamaduni wangu nilioukulia.

Mwanzoni nilidhani suala hilo lilikuwa ni langu pekee yangu. Nilipoendelea kukaa Chuoni, walikuja Watanzania wengine kujiunga na Chuo. Tukiwa kwenye mazungumzo na mawasilisho mbalimbali ya hoja za kitaaluma bado Watanzania wenzangu walionekana kuwa na shida kubwa katika kuitumia lugha ya Kiiingereza kwa ajili hiyo.

Nililazimika kujifunza jinsi Watanzania walivyoitumia lugha ya Kiingereza hata katika vitivo vingine tofauti na kile nilichokuwako mimi. Tatizo lilionekana kuwa ni hilo hilo. Kwangu mimi hili lilionesha kuwa Kiswahili ni lugha ambayo Watanzania tungeweza kuelewa na kufanya vizuri masomo kuliko lugha nyingine yoyote ile.
Zaidi sana, nilipojaribu kuchunguza kwa ufupi matumizi ya Lugha katika vyuo vilivyo vingi huko Ulaya, niliona kuwa vyuo hivyo viliyo vingi hufundisha kwa lugha zao. Kwa mfano Vyuo Vikuu katika nchi za Scandinavia, vyuo Vikuu vya Ufaransa, Ujerumani , nk., kwa sehemu kubwa hufundisha kwa lugha zao.

Swali kwangu likaja: Je ni kwa nini nchi hizi hukaza lugha zao zaidi katika kujifunzia, na siyo lugha za mataifa mengine? Kwa nini mtu akitaka kusoma katika vyuo hivi lazima ajifunze lugha ya kwao na siyo lugha nyingine. Jibu la haraka nililolipata ni kwamba vyuo hivi vinataka kukuza uelewa thabiti kwa wanafunzi wao juu ya yale wanayofundishwa, na siyo kuwafanya wanafunzi wakariri tu ili waweze kujibu mitihani.

Kwa hakika yapo mambo mengi, yanayokifanya Kiswahili kihitajike katika Elimu ya juu. Mambo haya matatu nimeyataja hapa ili kuwaambia ninyi waandishi wa habari na Watanzania wenzangu wote kwamba lugha hii ya Kiswahili ni lugha yetu, ni lugha ambayo ambayo kwa hakika itaweza kutusaidia sana kuzielewa nyanja mbalimbali za Taaluma kulingana na mazingira yetu.

Vitabu vilivyo vingi vya Kiingereza ambavyo hutumika kufundishia katika Elimu ya Juu havijaandikwa na Watanzania; vimeandikwa na wageni, tena katika mazingira ya kigeni. Kitabu kiki JIFUNZE UTAFITI kimeandikwa na Mtanzania mwenzenu, katika mazingira ya Kitanzania, tena  kwa lugha ambayo Mtanzania ataweza kuielewa vizuri.

Hata hivyo, ninapoeleza juu ya umuhimu wa kitabu hiki natambua fika silka tuliyo nayo Watanzania tulio wengi ya kudhamini vitu vya kigeni na kudharau vitu vyetu wenyewe. Hilo ninalitambua fika. Watu tulio wengi huona kuwa kitabu kilichoandikwa na Mzungu ni bora zaidi kuliko kile kilichoandikwa na Mwafrika, hata kama cha Mwafrika kina mambo mazuri ndani yake kuliko kile kilichoandikwa na Mzungu. Silka hii siyo kwa vitabu tu, bali ni katika vitu vingi. Ukweli huu unaeleweka, na utabakia hivyo,  hata kama hauwezi kukubaliwa na watu wote. Kwa hakika hili tulione kuwa ni tatizo, na kwamba hatuhitaji kuliendekeza.

Ninawaalika wanataaluma mbalimbali hapa Tanzania na nchi zingine zinazotumia Kiswahili kukisoma kitabu hiki, na pia kukuza Taaluma ya juu katika kuandika vitabu na makala mbalimbali kwa Lugha yetu ya Kiswahili.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: