Na. Luppy Kung'alo, Polisi Dodoma.
Jeshi la Polisi Mkoani Dodoma linawashikilia watuhumiwa tisa wa utapeli wanaojifanya Waganga wa Jadi na Tiba Asilia kwa kuwalaghai wananchi katika vijiji mbalimbali kisha kuwatapeli na kusababisha hofu, na uvunjifu wa Amani miongoni mwa wanakijiji mkoani humo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Bw. Zelothe Stephen alisema watuhumiwa hao wanajiita LAMBA LAMBA walikamatwa juzi katika Wilaya ya Kongwa, katika kijiji cha Mkoka baada ya Polisi kupata taarifa kuwa, wanakijiji hicho kuwavamia katika nyumba waliyofikia na kutaka kuwauwa.
”Matapeli hawa wametokea Mikoa ya Pwani, Dar es Salaam na Marogoro, na kuvamia mkoa wetu, kisha kufanya utapeli wao na kuzusha hali ya hofu na isiyo ya kawaida kwa wanakijiji wa maeneo mbalimbali ya mkoa wa Dodoma”. Alisisitiza Kamanda Zelothe Stephen.
Aidha Mkuu huyo wa Polisi Mkoa wa Dodoma alisema, Kundi hilo la LAMBA LAMBA limekuwa likichochea Chuki na Uadui miongoni mwa wanajamii kwa kufanya vitendo vya kupandikiza vitu nyakati za usiku, halafu baadae mchana wanakwenda kuvifukua na kudai wanabaini wachawi na kutoa uchawi katika kila nyumba kwa madai ya kualikwa na wazee wa Kimila.
Kamanda Zelothe Stephen alisema Matapeli hao, wamedai kualikwa na wazee wa kimila chini ya Mwenyekiti na Katibu waitwao SAMANDARO S/O? Na CHIPENDWA S/O? Na kupewa makazi katika nyumba mbili za ukoo wa MAPUGA S/O? Ambazo zinasimamiwa na Bw. SOSPETER S/O MAPUGA.
Akizungumza moja ya tukio lilozua hofu na kusababisha uvunjifu wa amani alisema katika shuguli zao walipita kila nyumba katika kijiji walichodai kualikwa na wazee hao lakini walipofika katika nyumba ya MESHACK s/o MAPUGA aliwakatilia kuingia kwake hivyo waliondoka kwenda katika vijiji vingine.
Alisema Baada ya kuondoka hapo Mtoto wa Mzee MESHACK S/O MAPUGA aitwaye MARTHA S/O AINEA MAPUGA MIAKA (34) mgogo mkazi wa kijiji cha Mlanje alianza kuumwa tumbo kisha kupelekwa zahanati ya Mkoka na hatimaye Hospitali ya wilaya Kongwa ambapo madaktari walithibitisha kifo cha binti huyo kutohusiana na imani za kishirikina lakini kwa bahati mbaya alifarikia dunia usiku wa tarehe 10/06/2012 akiwa Hospitalini hapa.
”Kifo hicho kilileta sintofahamu katika familia hiyo, iliyopelekea kufikiri kwamba kikundi cha LAMBA LAMBA walihusika na kwamba ndio tatizo kwa sababu za imani kishirikina.”aliongeza Bw, Zelothe Stephen.
Mkuu huyo wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma alisema kutokana na hali hiyo wanakijiji waliungana na familia ya wafiwa na kwenda kuwavamia kundi la LAMBA LAMBA wakiwa na silaha za jadi, ambazo ni mikuki, mapanga na marungu kwa lengo la kutaka kuwaua lakini walifanikiwa kuvunja mlango na madirisha na kukuta wametoroka.
Baadhi ya wanakijiji walitoa taarifa za tukio hilo kwa Jeshi la Polisi na Operesheni ya kuwatafuta watu hao ilianza ambapo jumla ya watuhumiwa saba kati ya tisa wa kundi hilo walikamatwa usiku huo na wengine wawili walikamatwa siku iliyofuta wakiwa wanawafuatilia wenzao, alisema Kamanda Zelothe.
Bw. Zelothe Stepen alisistiza kwamba pindi upelelezi utakapo kamilika watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani kujibu mashtaka yanayowakabili.
Hata hivyo Kamanda Zelothe alisema, Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma limeunda Kikosi kazi Maalumu katika wilaya zake zote kwa lengo la kufanya Operesheni Maalum ili kudhibiti na kutokomeza kundi hilo na washirika wake na kuahidi kuwasiliana na Makamanda wenzake wa mikoa ili kudhibiti vitendo hivyo.
”Napenda kutoa wito kwa wananchi wote, viongozi wa Serikali katika ngazi za Vijiji, Kata, Tarafa na Wilaya kusimamia Sheria, Kanuni na taratibu za nchi zinavyotaka, ili kuweza kudhibiti uhalifu huu na kuondoa hali ya sintofahami miongoni mwa jamii inayoweza kusababisha uvunjifu wa Amani ndani na nje ya mkoa wa Dodoma inatokomezwa.” Alisistiza kamanda Zelothe Steven.
Toa Maoni Yako:
0 comments: