Na Luppy Kung’alo wa Jeshi la Polisi Dodoma
Jeshi la Polisi Mkoani Dodoma linamshikilia mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la RAMADHANI S/O AMIR Mwenye umri wa miaka 24, Mkulima na Mkazi wa Pahi wilayani Kondoa kwa tuhuma za mauaji.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Bw. Zelothe Stephen alisema tukio hilo la mauaji lilitokea tarehe 17/06/2012 majira ya saa 17:15 jioni katika kitongoji cha Lusangi Kijiji na Tarafa ya Pahi Wilaya ya Kondoa Mkoani Dodom.
Akizungumzia tukio hilo alisema kwamba mtuhumiwa huyo alimshambulia na kumpiga bwana MOHAMED S/O IBRAHIM Mwenye umri wa miaka 60, Mkulima na Mkazi wa Lusangi kwa kumpiga na kipande cha kuni kichwani na kisha kumchoma na kitu chenye ncha kali kifuani.
“Marehemu alikuwa nyumbani kwake na mara ghafla akatokea mtuhumiwa huyo na kuanza kumpiga na kumshambulia.” Alisema Kamanda Zelothe Stephen
Bw. Zelothe alisema kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa na majirani wa eneo hilo walidai kwamba mtuhumiwa ni mgonjwa wa akili, hata hivyo mtuhumiwa amekamatwa na atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili.
Mkuu huyo wa Polisi Mkoa wa Dodoma alisema Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti katika Hospitali ya Wilaya ya Kondoa.
Wakati huo huo mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la la MASUMBUKO S/O JACKSON Mwenye umri wa miaka 25, Mlinzi katika Kanisa Katoliki la K/Ndege na Mkazi wa Mailimbili amefariki Dunia katika tukio la ajali ya gari kugongana na pikipiki aina ya bajaji.
Akizungumzia tukio hilo Kamanda Zelothe Stephen alisema lilitokea tarehe 17/06/2012 Majira ya saa 21:30 usiku maeneo ya Kiwanja cha Mpira wa Miguu cha Dodoma (Jamuhuri Stadium) Barabara ya Mpwapwa,
Alisema gari lenye namba za usajili T.220 AVR Toyota Land Cruiser likiendeshwa na dereva asiyefahamika likitokea soko la Miembeni likielekea eneo la Ndasha liligongana na Pikipiki namba T.416 BPJ Bajaji iliyokuwaikiendeshwa na ELIAS S/O BONIFASI Mwenye umri wa miaka 35, Mkazi wa Mailimbili.
Bw. Zelothe Stephen alisema ajali hiyo ilisababisha kifo kwa abiria wa Pikipiki hiyo aliyetambulika kwa jina la MASUMBUKO S/O JACKSON Mwenye umri wa miaka 25, Mlinzi katika Kanisa Katoliki la Kiwanja cha Ndege, Mkazi wa Mailimbili.
Kamanda Zelothe alisema Chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa Dereva wa Pikipiki kwani alipaswa kusimama kabla ya kuvuka barabara hiyo.
Dereva wa gari hilo amekimbia baada ya kusababisha ajali hiyo na Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma linaendelea kumtafuta ili kumtia mbaroni.
Alisema Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma.
Katika tukio linguine Kamanda Zelothe alisema mnamo tarehe 16/06/2012 majira ya saa 19:00 Jioni, maeneo ya Chang’ombe Manispaa ya Dodoma, gari lenye namba za usajili T.432 AHH Toyota Hiace lililokuwa likiendeshwa na Dereva asiyefahamika lilimgonga mpanda baiskeli na kusababisha kifo.
Mkuu huyo wa Polisi Mkoa wa Dodoma alisema Mpanda Baiskeli huyo ametambulika kwa jina la BARTON S/O PAUL Mwenye umri wa miaka 54, Mlinzi wa Ajope Security Guard, Mkazi wa Chang’ombe.
“Mpanda Baiskeli huyo alifariki siku iliyofuata majira ya saa 12:15 Mchana akiwa anaendelea kupata matibabu katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma Wodi namba 10.”Aliongeza Bw. Zelothe Stephen
Kamanda Zelothe alisema Dereva wa gari hilo amekimbia baada ya kusababisha ajali hiyo na Jeshi la Polisi Mkoa Dodoma linaendelea kumsaka.
Alisema uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa Dereva kwa kutokuwa muangalifu kwa watumiaji wengine wa barabara.
Aidha Mwili wa marehemu umekabidhiwa kwa wanandugu tayari kwa mazishi.
Toa Maoni Yako:
0 comments: