MASHINDANO ya Kombe la Kagame, yamepangwa kuanza kutimua vumbi Julai 14 hadi 29 mwaka huu, huku mguso na uzalendo wa kweli kwa mashabiki wa Tanzania, kuwa chachu ya kuyafanya mashindano hayo yaendelee kufanyika nchini, huku timu zinazotaka kushiriki zikitakiwa zijilipie nauli ya kuja na kurudi.

Hali hiyo imechangiwa na ukata kwa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati pamoja na wasimamizi wakuu, ambao ni Shirikisho la Soka nchini (TFF), jambo linalochangiwa kwa kiasi kikubwa na ukosefu wa wadhamini wa kutosha.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Michezo Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Leodegar Tenga, alisema moyo wa uzalendo pamoja na kupenda michezo kwa mashabiki wa Tanzania, ni ishara tosha ya kuyafanya mashindano hayo yafanyike kwa mafanikio.

Tenga alisema hadi sasa hawajapata wadhamini hivyo wanaendeleza juhudi zao, ili kuhakikisha kwamba mashindano hayo yanakuwa na chachu na mafanikio makubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

“Tumekubaliana na Wajumbe wa CECAFA kwa kuwa mashindano hayo hayana udhamini, basi timu zote zijigharamie usafiri wa kuja na kuondoka Dar es Salaam, huku TFF wao wakihakikisha kwamba yanaendelea kufanyika na kugharamia mambo mengine.

“Tunafuraha kwa mashindano haya kufanyika tena Tanzania, kwakuwa pamoja na kupata fursa ya kuuhamasisha mchezo wa soka, lakini pia inatoa fursa kwa timu nyingi za Tanzania kushiriki na kujitangaza kimataifa,” alisema.

Tenga alisema wanafanya mazungumzo na Televisheni ya kulipia ya Super Sport na nyingine ili zionyeshe mashindano hayo moja kwa moja, huku juhudi kubwa za wadau zikiwekwa kwa ajili ya kuyachangia mashindano hayo.

Kwa Tanzania, timu za Yanga SC, Simba SC na Azam FC, wataingia uwanjani kuiwakilisha nchi katika mashindano hayo makubwa Afrika Mashariki na Kati, huku timu nne kutoka nje ya ukanda huu ambazo ni Vita Club ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Dymanos ya Zimbabwe na Blomomfontein na Platinum za Afrika Kusini, zikiomba kushiriki michuano hiyo.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: