SERIKALI imekabidhi sh. milioni 10 kwa mama mzazi wa aliyekuwa nguli wa filamu nchini, Steven Kanumba, Frola Mtegoa kama rambi rambi ya msiba huo.
Akizungumza wakati akikabidhi fedha hizo nyumbani kwa marehemu, Kanumba, Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makalla alisema Serikali inatambua mchango wa Kanumba katika tasnia ya sanaa ya filamu na maigizo hapa nchini.
Alisema kifo chake kimeipa Serikali changamoto kubwa ya kuhakikisha inalinda na kusimamia vyema kazi za wasanii, hivyo mchakato huo utaenda kwa kasi sana.
"Kifo chake ni changamoto kubwa kwetu hivyo kutokana na cheo changu nitahakikisha naipeleka kasi mchakato wa kulinda kazi za wasanii ili ifike mahala kila msanii aridhike na anachokipata, kwani marehemu Kanumba aliigiza filamu nyingi lakini hakupata mafanikio kama ilivyotakiwa" alisema Makala.
Alisema Serikali kwa kushirikiana vema na Kamati ya mazishi iliyokuwa ikiongozwa na Gabriel Mtitu, wametoa fedha hizo ambazo Serikali iliahidi kutoa kwa ajili ya rambi rambi ya marehemu Kanumba aliyeweza kuinua na kuitangaza tasnia ya filamu nchini.
"Nakumbuka nilienda nchini Uingereza kufungua tawi la Chama Cha Mapinduzi (CCM) nilishangaa sana kumkuta Kanumba huko akiwa na Mkrugenzi wa Bendi ya Twanga Pepeta, Asha Baraka wakiwa wanahamasisha Watanzania waishio huko kuhusiana na chama, hivyo wanaosema Kanumba ni alikuwa si mwanachama wa CCM naomba niwaeleze kuwa si kweli" alisema Makalla.
Naye mama mzazi wa Kanumba, Frola alitoa shukrani kwa Serikali kwani amefarijika na kuona kwamba Serikali inamjali licha ua kumpoteza mwanae kipenzi.
"Kwa kweli naishukuru sana Serikali kwani wamenifariji sana, Japo Kanumba hatorudi tena lakini nimefarijika kwa ushirikiano mlionipa" alisema mama mzazi wa Kanumba.
Wakati huohuo Mtitu alitoa shukrani kwa Serikali kwani mchango waliotoa unaonyesha kwamba wanatambua kazi za wasanii hapa nchini.
"Kwa jina alilokuwa nalo Kanumba pamoja na filamu alizoigiza, hakupaswa kuwa vile ndio mana hata kwenye msiba nilisema marehemu aliondoka akiwa masikini, hivyo tunashukuru kwamba Serikali imetambua na imetuhakikishia kulinda kazi zetu ili na sisi tule kutokana na jasho letu" alisema Mtitu.
Toa Maoni Yako:
0 comments: