Makamu Mkuu Shule ya Sekondari Kivesa, Faustine Mrosso, shule hiyo iliyopo Kata ya Chanika inahudumia vijiji vya Kwediyamba, Kwedizando na Kwekambara maeneo ambayo ni mbali na shule hiyo.
Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Kata ya Komnyang'anyo wakitembea barabarani kuelekea kwenye makazi yao vijiji mbalimbali vinavyoizunguka shule hiyo.
---
Na Joachim Mushi, Thehabari.com- Handeni

WANANCHI wilayani Handeni wameilalamikia mazingira magumu kimiundombinu ya shule za sekondari za kata katika wilaya hilo na kudai ndiyo chanzo cha kuongezeka kwa mimba kwa wanafunzi na kukatisha masomo.

Kauli hiyo imetolewa kwa nyakati tofauti katika mahojiano ya baadhi ya wakazi wa Handeni na mwandishi wa habari hizi ndani ya uchunguzi uliofanywa hivi karibuni maeneo anuai ya wilaya hiyo kwa ushirikiano na Chama cha Wanahabari Wanawake (TAMWA).

Abdulah Mwamponda Mkazi wa Kijiji cha Msasa, wilayani Handeni alisema shule nyingi za kata zimejengwa mbali na makazi ya wanafunzi jambo ambalo linawapa mzigo wazazi na wanafunzi kujitafutia usafiri wa kwenda na kurudi shuleni.

Alisema katika kijiji hicho wapo wanafunzi ambao hutembea umbali wa kilometa 12 na hata 20 kila siku kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa kwenda na kurudi shuleni, umbali ambao umekuwa na vishawishi vingi hasa kwa wanafunzi wa kike kiusafiri.

 Alisema usafiri katika vijiji hivyo ni wa baiskeli na pikipiki (bodaboda) ambao wazazi wengi wanashindwa kugharamia hivyo watoto kutembea kwa umbali huo, huku wakati mwingine wakishawishika kupewa msaada wa lifti na madereva wa bodaboda ambao baadaye huanza kushirikiana nao kimapenzi.

Mzazi Fatuma Shaban kutoka Kijiji cha Komnyang’anyo alisema wanafunzi wengi huondoka nyumbani kwao saa 10 za asubuhi na kurudi usiku kutokana na umbali huo huku wengine wakishinda shuleni bila chochote kutokana na uduni wa maisha ya kaya nyingi eneo hilo.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Kilimani, Rajab Nyange alisema katika shule hiyo iliyopo Kata ya Vibaoni nje kidogo ya Mji wa Handeni wapo wanafunzi wanaotoka vijiji vya mbali takribani kilimeta sita hadi 10 kutoka nyumbani kwao, ambao hutembea kilomita 20 kila siku yaani kwenda na kurudi shuleni jambo ambalo linaibua vishawishi kwa wanafunzi.

“Mzazi anashindwa hata kumpa mtoto wake sh. 100 au 200 kila siku ya shule kwa ajili ya kula chochote awapo shuleni, je ataweza kumlipia mtoto huyo gharama za usafiri ambazo ni za juu zaidi kutokana na umbali kutoka kijiji kimoja hadi kingine,” alihoji Nyange.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Hassan Mwachibuzi anasema Ofisi yake haina taarifa za ubakaji wa moja kwa moja japokuwa anakiri kuwepo kwa vitendo vya utoro kwa wanafunzi wote kwa sababu mbalimbali. Anasema pamoja na hayo utoro waweza kuingiliana na ukatishwaji masomo kwa mimba.

Kiongozi huyu anakiri suala la umbali wa shule huchangia vishawishi kadhaa vya wanafunzi hasa wa kike kukumbwa na vikwazo kadhaa katika masomo yao. Hata hivyo anabainisha kuwa uongozi unajitahidi kulitatua suala hilo kwa kuongeza ujenzi wa hosteli kwa wanafunzi katika shule za kata ili wanafunzi waondokane na vikwavyo anuai.

Aliongeza kuwa tayari wamejenga hosteli katika maeneo ya Kisasa, Kwamsisi, Misima, na kudai kuwa wanaendelea maeneo mengine kwa kushirikiana na wananchi na wahisani huku lengo ni kuhakikisha kila kata inakuwa na hosteli zake kwa ajili ya wanafunzi wanaotoka maeneo ya mbali na shule.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: