Habari: Boniface Meena Gazeti la Mwananchi. 

BUNGE la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, jana liliwachagua Watanzania tisa kuingia katika Bunge la Afrika Mashariki (EALA), katika uchaguzi uliofanyika mjini Dodoma.

Katika uchaguzi huo, Twaha Taslima wa Cuf na Nderakindo Kessy wa NCCR-Mageuzi walichaguliwa kwa upande wa vyama vya upinzani. Taslima alipata kura 175 na Kessy kura 113.

Kabla ya uchaguzi wa jana, upinzani ulikuwa na nafasi moja katika bunge hilo ambayo ilikuwa inashikiliwa na Dk Fortunatus Masha wa UDP ambaye alianguka baada ya kupata kura 58.

Kwa upande wa wagombea wa CCM, Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Mara, Charles Makongoro Nyerere, Meneja Uhusiano wa Benki ya NMB, Shy-Rose Bhanji (Pichani) na Katibu Mkuu wa Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania, Adam Kimbisa walishinda.

Akitangaza matokeo hayo Msimamizi wa Uchaguzi huo ambaye pia ni Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashilillah alisema Bhanji alishika nafasi ya pili katika kundi la kwanza (wanawake) akipata kura 120 akitanguliwa na Angela Kizigha aliyepata kura 166. Wote ni kutoka CCM.

Wengine waliogombea katika kundi hilo ni Rose Mwalusamba wa CUF ambaye licha ya kujitoa alipata kura saba, Fancy Haji Nkuhi (57), Dk Goodbertha Kinyondo (32), Janet Mmari (119) na Janet Mbene (87).

Katika kundi la pili kutoka Zanzibar, Abdullah Ali Hassan Mwinyi alirejea tena katika bunge hilo baada ya kuongoza kwa kupata kura 227 akifuatiwa na Mariam Ussi Yahya (91).

Katika kundi hilo, Septuu Nassor Mohammed na Dk Said Gharib Billal () walishindwa kurejea katika bunge hilo baada ya kuambulia kura 74 na 88 mtawalia. Wengine walioshindwa ni Dk Ahmada Hamid Khatibu (36), Dk Haji Mwita Haji (11), Khamisi Jabir Makame (6) na Zubeir Ali Maulid (39).

Katika kundi la vyama vya upinzani, mbali ya Dk Masha wengine walioshindwa ni Anthony Komu wa Chadema (93), Juju Danda wa NCCR-Mageuzi (23), Micah Mrindoko wa TLP (66) na Mwaiseje Polisya wa NCCR-Mageuzi (42).

Katika kundi la nne la Tanzania Bara, Kimbisa ambaye aliwahi kuwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam aliongoza kwa kupata kura 210 akifuatiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa zamani wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Bernard Murunya aliyepata kura 135 na Makongoro kura 123.

Walioshindwa katika kundi hilo ni Dk Edmund Mndolwa (42), Elibariki Kingu (31), Dk Evans Rwaikiza (78), Mrisho Gambo (75) na Siraju Kaboyonga (38) wote kutoka CCM na John Lifa Chipaka wa Tadea (8).
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: