Na Mohammed Mhina, wa Jeshi la Polisi Zanzibar
Jeshi la Polisi Zanzibar leo limepokea msaada wa pikipiki kumi kutoka Kampuni ya Simu za Mkononi ya Zantel ili kusaidia kutatua tatizo la usafiri kwa Jeshi hilo.
Akikabidhi pikpiki hizo kwa niaba ya kampuni ya Zantel, Afisa masoko wa kampuni hiyo Bw. Mohammed Mussa, amesema kuwa kampuni yake imeamua kutoa msaada huo ili kuwawezesha askari Polisi kuweza kufika kwa haraka katika maeneo ya matukio.
Amesema Kampuni yake inafahamu upungufu wa vitendea kazi unaolikabili Jeshi la Polisi na kwamba wameona kuna umuhimu wa wao kama Kampuni kulisaidia Jeshi hilo ili liweze kuwahudumia wananchi kwa haraka zaidi.
Aidha Kamuni hiyo pia imeahidi kuendelea kulisaidia Jeshi la Polisi katika masuala ya mawasiliano kama vile radio za mikononi ili kuvisaidia vikundi vya ulinzi shirikishi katika maeneo mbalimbali visiwani humo.
Akipokea msaada huo, Mkuu wa Utawala wa Jeshi la Polisi Zanzibar Kamishna Msaidizi Mwandamizi SACP Keneth Kaseke, amesema pikipiki hizo zitasaidi kwa kiasi kikubwa katika kukabiliana na matukio ya kihalifu hasa katika maeneo yenye barabara finyu ya Mji Mkongwe.
Kamanda Kaseke alikuwa amemwakilisha Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar CP Mussa Ali Mussa, katika hafla hiyo ya kupokea msaada huo wa pikpiki kumi aina ya MTR zenyethamani ya shilingi milioni 17.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo iliyofanyika Makao makuu ya Jeshi la Polisi Zanzibar, Kamanda Kaseke ameishukuru kampuni hiyo ya Zantel kwa msaada huo na isichoke kuendelea kulisaidia Jeshi hilo katika nyanja nyingine.
Kamanda kaseke pia ametoa wito kwa Makampuni mengine hapa nchini kujitolea kulisaidia Jeshi la Polisi katiak kupata misaada mbalimbali kwani amesema bado Jeshi hilo linakabiliwa na upungufu mkubwa wa vitendea kazi pamoja na samani za ofisi.
Toa Maoni Yako:
0 comments: