Na Pardon Mbwate na Felister, wa Jeshi la Polisi -Kigoma

JESHI la Polisi mkoani Kigoma leo limewafukuza kazi askari wake wanne kwa tuhuma za kudai na kupokea rushwa ya dola 300 za Kimarekani kutoka kwa raia mmoja wa China kinyume na maadili ya Jeshi hilo.

Kamanda wa Polisi mkoani Kigoma Frasser Kashai (pichani) amewataja askari waliohukuzwa kazi kuwa ni mwenye namba E.3890 CPL Admirabils Malaso(43), G. 814 PC Waziri Juma Rashidi(30) G. 3012 PC Makasi Edwin(25) na  G. 3322 PC Elias Zakaria(24) ambao wote walikuwa wakifanyia kazi katika kituo cha Polisi Uvinza wilaya ya Kigoma Vijijini.

Kamanda Kashai amesema kuwa mnamo Aprili 1, 2012 majira ya saa 5.00 usiku askari hao wakiwa zamu katika kituo hicho cha Polisi Uvinza, walipokea taarifa kwa njia ya simu ya mkononi kutoka kwa dada mmoja aitwaye Mary Kapele(26) akiwaeleza kuwa yuko katika nyumba moja ya kulala wageni ya Manchester na alikuwa na Raia mmoja wa Kichina mmoja wa wasimamizi wa ujenzi wa barabara ya kutoka Kigoma Uvinza na kwamba waende kumshika ugoni ili wajipatie fedha na baadaye kugawana na dada huyo.

Askari hao walikwenda katika nyumba hiyo ya kulala wageni na kumkamata Mchina huyo aitwaye Mafutao War, akiwa pamoja na dada huyo kisha wakamtaka atoe fedha kama malipo ya kumshika ugoni na ndipo walipopewa kiasi cha dola 300 za kimarekani na shilingi 10,000 za Kitanzania na kumuachia. Kamanda kashai amesema kuwa mlalamikaji Bw. War alikuwa ni mkandarasi wa kampuni ya ujenzi ya Chico inayojenga barabara ya kutoka Kigoma Uvinza.]

Kamanda Kashai alisema baada ya kuona tukio hilo, raia wema walitoa taarifa Polisi mkoani Kigoma ambapo askari hao walikamatwa na baada ya uchunguzi kufanyika walibainika kuwa walihusika na tukio hilo na ndipo waliposhitakiwa kijeshi na kupatikana na hatia ya kufanya Kitendo kibaya kinyume na mwenendo mwema wa Jeshi la Polisi.

Amesema kufuatia hukumu hiyo ameamua kuwafukuza kazi kwa fedheha ili iwe fundishi kwa askari wengine kufuata utaratibu na sheria katika utendaji wa kazi zao za kila siku.

Kamanda Kashai amesema Koplo Admirabils Malalo ambaye alizaliwa Julai 1, 1969 katika kijiji cha Kilando wialaya ya Nkasi mkoani Rukwa,   alijiunga na Jeshi la Polisi Julai 26, 1991 na hadi anafukuzwa amelitumikia Jeshi hilo kwa muda wa miaka 11, Kostebo Waziri Juma Rashidi alizaliwa  Julai 1, 1982 katika kijiji cha Maisaka wilaya ya Babati mkoani Manyara, na alijiunga na Jeshi la Polisi Februari  05, 2007 na hadi kufukuzwa kwake alikuwa amelitumikia Jeshi la Polisi kwa muda wa miaka mitano.

Amesema Konstebo Makasi Edwin ambaye alizaliwa Februari 28, 1987 huko kwenye eneo eneo la Mabatini mjini Mwanza la na kujiunga na Jeshi la Polisi Juni 28, 2009 amelitumikia Jeshi hilo kwa muda wa miaka mitatu na Konstebo Elias Zakaria ambaye alizaliwa  mwaka Julai 1, 1988 huko katika eneo la Nguvumali mjini Tanga na alijiunga na Jeshi la Polisi Juni 28, 2009 ambaye naye pia amelitumia Jeshi hilo kwa muda wa miaka mitatu tu.

Kamanda kashai amesema kuwa Jeshi la Polisi halitasita kumchukulia hatua kali za kisheria na hata kumfukuza kazi askari yeyote atakayebainika kwenda kinyume na maadili ya Jeshi hilo iki ni pamoja na kujihusisha na vitendo vya utovu wa nidhamu, uhalifu ukiwemo wa kudai na kupokea rushwa.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: