Baadhi ya walimu waliopo katika mafunzo ya vitendo katika Kituo cha Walemavu cha Shule ya Msingi Iliboru wakifundisha darasa la nne.
Baadhi ya wanafunzi wa darasa la nne (viziwi) katika Kituo cha Walemavu cha Shule ya Msingi Iliboru wakiandika darasani.
Na Joachim Mushi, Thehabari.com-Arumeru
BAADHI ya walimu wa wanafunzi wenye ulemavu anuai wilayani
hapa wameitaka Serikali kuacha utaratibu wa kuwataini wanafunzi wenye ulemavu
katika mitihani ya taifa kwa vigezo sawa hasa upande wa muda wa kufanya
mitihani husika.
Wamesema hali hiyo inawanyima baadhi ya wanafunzi
wenyeulemavu kujipima kiusahihi kutokana na dosari zao na wanafunzi wa kawaida
hivyo kujikuta wengi wakifanya vibaya au kutopata daraja stahili kwenye
matokeo.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana mjini hapa,
Mwalimu Mkuu wa Kituo cha Wanafunzi wenye ulemavu, Shule ya Msingi Naurei
wilayani Arumeru, Tuzie Mtenga amesema kitendo cha kuwachanganya wanafunzi hao
baadhi yao wameishia kufanya vibaya katika
masomo yao hasa
kwenye mitiani ya mwisho kitaifa.
“Mwanafunzi mwenye ulemavu baada ya kumaliza mafunzo kwenye
vitengo vyao tumekuwa tukiwachanganya kwenye madarasa ya kawaida shule za
msingi, wanaendelea na baadaye wanafanya mitihani ya taifa kwa muda sawa na
wengine hiki si kipimo sahihi kwa kweli,” alisema Mtenga ambaye kituo chake
kinawalemavu wa akili na viungo.
Naye mwalimu, Rams Mosha wa Chuo cha Mafunzo kwa Watu wenye
Ulemavu Usa River amesema wapo wanafunzi wenye ulemavu ambao kasi yao ya
uandishi ni tofauti na mwanafunzi wa kawaida na wanauelewa lakini wamekuwa
hawapati haki pale wanapotahiniwa kwa vigezo sawa hasa muda na wanafunzi
wengine.
“Walemavu wengine wanaandika huku wakitetemeka sasa mtu kama
huyu waweza kukuta anafanya vizuri darasani lakini kwa kuwa baadaye anafanya
mtihani wa taifa kwa muda sawa na watahiniwa wa kawaida anaweza asimalize
mtihani au kutofanya vizuri…hili aliangaliwi na mamlaka husika,” alisema Mosha
ambaye naye ni mlemavu wa viungo.
Kwa upande wake Mwalimu Mratibu wa Kituo cha Walemavu cha
Shule ya Msingi Iliboru, Loitusho Yamat ipo haja ya wanafunzi walemavu
kufuatiliwa kwa karibu tofauti na ilivyo sasa ambapo wengi wameshindwa kufanya
vizuri kutokana na usimamizi afifu uliopo kielimu.
Yamat ambaye shule yake ina jumla ya wanafunzi walemavu 60,
yaani wanafunzi viziwi na wale wenye mtindio wa ubongo alisema kwa sasa kituo
hicho kimetafuta ufadhili kwa ajili ya ujenzi wa shule ndogo ya sekondari kwa
wanafunzi wenye ulemavu ili kuwafuatilia kwa karibu baada ya masomo ya msingi.
Habari na picha zote
zimeandaliwa na mtandao wa Thehabari.com kwa ushirikiano na Kituo cha Habari
Kuhusu Ulemavu Tanzania
(ICD)



Toa Maoni Yako:
0 comments: