Isha Ramadhani ni mmoja wa wasanii wa muziki wa taarab nchini ambaye kwa sasa anafanya vizuri sana katika tasnia hiyo. Na kuna baadhi ya wasanii wa muziki huo wameshaanza kuonyesha dalili za wivu kutokana na mafanikio aliyonayo mpaka sasa.

Msanii huyo ambaye kipaji chake kilianza toka akiwa mwanafunzi katika Shule ya Msingi Mnazi Mmoja, ambapo alihitimu mwaka 1997 na kujiunga na Shule ya Sekondari hata hivyo aliishia kidato cha pili.

Anasema kuwa alikuwa ana hamu sana ya kusoma lakini kutokana na wazazi wake kutokuwa na uwezo, alikatisha masomo yake mwaka 1999 wakati akiwa kidato cha pili. Isha anasema kuwa aliamua kujiunga na muziki wa taarab baada ya kuona kuwa ana kipaji tangu akiwa mdogo. Kutokana na kupenda nyimbo mbalimbali alizokuwa anaimba mama yake, aliona kuwa bora ajikite katika muziki huo ambao aliona kuwa utamsaidia baadaye.

Isha ambaye alizaliwa mwaka 1980, amefuata nyazo za Mama yake Rukia Juma ambaye alianza kuimba muziki wa taarab katika bendi ya Babilon mwaka 1997 na baadaye akajiunga na TOT Taarab ambapo anaimba mpaka sasa.

Isha alianza kuimba muziki katika bendi ya Segere, iliyopo Sinza, na baadaye mwaka 2005 akajiunga katika bendi ya Jahazi ambayo inaongozwa na Mzee Yusuph.

Baadaye alijikuta amehamia katika bendi ya muziki huo huo ya TOT Modern kwa ajili ya kumfuata Mama yake lakini mwaka 2008 akaamua kurudi Jahazi.


Na baadaye aliona kuwa ana uwezo wa kuimba nyimbo mwenyewe na katika kujaribu akamshirikisha Mama yake na kutoa wimbo wa kwanza kabisa uliokwenda kwa jina la Mama Nipe Radhi.

“Muziki una mapungufu yake lakini kutokana na kuamua kuwa hiyo itakuwa ndio kazi yangu ya maisha niliamua kuwa nao nao makuni mpaka hapa nilipofika” anasema.


Anasema kuwa baada ya kutoa wimbo huo akiwa na Mama yake, alipata mialiko mbalimbali kwa ajili ya kufanya maonesho.

“Kikubwa kilichokuwa kinanipa moyo ni pale ninaposimama jukwaani na kuona mashabiki wakinishangilia kwa kupenda nyimbo  zangu” anasema.

Msanii huyo anasema baadaye alikaa na kutafakari akaona kuwa anaweza kuanzisha bendi yake na kuamua kuanzisha bendi yake ya Mashauzi Classic, ambayo mpaka sasa ameshakamilisha albamu mbili.

“Mafanikio makubwa niliyoyapata katika muziki wa taarabu ni pamoja na kukamilishja albamu zangu mbili ambapo nipo katika maandalizi ya mwisho kuziingiza sokoni” anasema.

Albamu ambazo zimekamilika ni pamoja na 'Si Bure Una Mapungufu' na Sijamwona Kati yenu ambapo ya kwanza inatoka mwezi Aprili mwaka huu.

Anasema kuwa albamu zote zina nyimbo nne nne kila moja ambazo zmezifanyia katika studio ya MA Records pamoja na Sounda Crafers.

“Albamu ya kwanza ya Si Bure Una Mapungufu,  ninatarajia kuiingiza sokoni Aprili mwaka huu na ya pili itafuatia” alisema.

Msanii huyo anasema kuwa matarajio yake ni kuitambulisha bendi yake Kimataifa hasa katika nchi za Ulaya, kutokana na kuwa na watanzania wengi wanaopenda kusikia na kuwaona wasanii wa nyumbani lakini kutokana na ubunifu duni wamekuwa wakishindwa kuvipata vitu hivyo kwa wakati.

“Mpango ilionao kwa sasa baada ya kizindua albamu ya kwanza, ninatarajia kuanza ziara kwa ajili ya kuitambulisha bendi kwenye nchi mbalimbali ambapo kwa kuanzia ntaanza Ugiriki, Uingereza na nchi za Kiarabu” alisema.

Anasema kuwa pia kutokana na kuanzisha bendi yake ya Mashauzi Clasic, amepata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kumiliki nyumba katika eneo la Mbezi Dar es Salaam ambapo ndio anapoishi na familia yake.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: