wanaharakati wa haki za binadamu
 kutoka mashirika mbali mbali ikiwepo Policy Forum, TGNP, LHRC, SIKIKA, TAMWA, HAKIARDHI, HAKIELIMU, GDSS, Jipange, ForDia, na FemAct wakitoa tamko lao kwa waandishi wa habari kuhusu kumalizika kwa mgogoro kati ya serikali na madaktari.
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la SIKIKA Bw. Irenei Kiria  akitilia mkazo maongezi yao na kusema kuwa ni vyema watendaji wa serikali kutambua utu ni kitu kizuri sana kuliko uongozi.
Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Bi. Usu Mallya akijibu maswali ya waandishi wa habari waliofika kusikiliza tamko lao.

Mkurugenzi wa Kituo cha Haki za Binadamu Dr. Hellen Kijo-Bisimba akiongea na waandishi wa habari juu ya tamko lao, kulia ni Mkurugenzi wa Tamwa Ananilea Nkya na kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Bi. Usu Mallya.

Mkurugenzi wa Kituo cha Haki za Binadamu Dr. Hellen Kijo-Bisimba akiongea na waandishi wa habari juu ya tamko lao.
 Mkurugenzi wa Tamwa Ananilea Nkya  akitilia mkazo tamko lao ambalo wamelitoa.
---
TAMKO KWA VYOMBO  VYA HABARI: KUHUSU KUMALIZIKA KWA MGOGORO KATI YA SERIKALI NA MADAKTARI 10.02.2012

Sisi wanaharakati wa haki za binadamu,baada ya kuzingatia kwa kina matukio,maamuzi na matokeo yaliyojiri  kwa kipindi cha takribani wiki tatu (Kuanzia Tarehe 21 Januari hadi 9 Februari  2012) za mgogoro kati ya madaktari nchini tumebaini;

1.Kuwa, Mgogoro huu umevunja haki ya kuishi kwa wananchi kadhaa na umehatarisha haki za raia wengi sana; inakadiriwa kuwa wananchi wengi wamekufa kwa kipindi hiki cha mgogoro huku wengi zaidi wakipata madhara yasiyorekebishika na huku maelfu wakiteseka na maumivu makali;

2.Kuwa, Serikali imeonesha udhaifu mkubwa katika kutumia mamlaka iliyopewa na wananchi, hususani wajibu wake wa kusimamia haki za binadamu; ikiwa ni pamoja na kutotoa maamuzi sahihi na kwa wakati na hivyo kusababisha madhara makubwa kwa jamii;

3.Kuwa, Serikali imeshindwa kutumia rasilimali tulizoikabidhi, kutatua tatizo hili huku ikifumbia macho matumizi mabaya na makubwa  ya fedha za umma ya maafisa na viongozi wa Wizara  ya Afya na Ustawi wa Jamii. Aidha viongozi wa Wizara hii wameshindwa kabisa kutoa uongozi stahiki kwa watendaji na madaktari ambao ndio watekelezaji na watoa huduma kwa jamii

4. Kuwa, Katiba inatoa jukumu la moja kwa moja kwa wananchi kuchukuwa hatua za kuiwajibisha Serikali kutekeleza wajibu wake; na kwamba, pale wananchi tulipochukua jukumu la kuikumbusha Serikali wajibu wake na kuitaka kuchukuwa hatua stahiki na za haraka kutatua matatizo haya, Serikali imechukuwa uamuzi wa kutumia mabavu kutukamata na kututisha. Siyo tu kuwa hii haikubaliki lakini pia ni ukiukwaji wa haki za binadamu na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

5.KUWA, majibu yaliyotolewa na Serikali kama hatua za kutatua mgogoro yameonyesha ishara ya nia njema ingawa yanahitaji utekelezaji wa kuaminika; pia tumebaini kuwa kinyume cha katiba ya  ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, kumekuwa na utamaduni wa uongozi wa juu kutowajibisha na kutowajibika kwa vitendo viovu kama hivi : Kwa maaana hii, kutokumwajibisha na kuwajibika kwa Waziri wa Afya na Naibu wake ni kinyume na kanuni za uwajibikaji na kulindana.

6.KUWA, Bunge ambalo ndilo msimamizi wa Serikali, halikuchukuwa hatua za haraka kuiwajibisha Serikali na kwa kuwa mwenendo wa Spika na Naibu Spika umejikita katika ufinyu wa kutafsiri kanuni kwa  ajili ya maslahi ya umma na uhai wa Watanzania;

7.Na KUWA, Ibara ya 26 ya Katiba inamtaka kila raia wa nchi hii kuilinda Katiba na sheria zingine za Nchi;

HIVYO BASI; Tunawasihi wananchi wenzetu kuwa,ni vema sasa tuchukue nafasi yetu kuitaka Serikali kuwajibika kwa madhara yaliyoyokea,kuikumbusha haya ya kuchukuwa hatua za ziada kurejesha hali ya kawaida kwenye hospitali za umma na kutekeleza ahadi zake kwa madaktari ;

1. Tunawataka Waziri wa Afya Haji Mponda na Naibu Waziri Lucy Nkya wajiuzulu mara moja kwa kushindwa kutatua mgogoro huu wa madaktari na kusababisha vifo na madhara makubwa kwa Watanzania . Ama sivyo tunamtaka Rais Jakaya Mrisho Kikwete awafukuze kazi haraka iwezekanavyo.

2. Waziri Mkuu autangazie umma, Ndani ya wiki moja ni hasara gani, ni madhara kiasi gani ambayo  wananchi na taifa limepata kwa kuingia kwenye mgogoro na madaktari.

3. Spika wa Bunge,auombe radhi umma juu ya hatua na kauli zake za kibabe Bungeni kuzima hoja za Wabunge kutafakari mgogoro huu huku akijua kuwa kwa kufanya hivyo ni kuendeleza maafa yaliyokuwa yanayowakumba watanzania.

4. Tume iliyounda kushughulikia tatizo hili itoe taarifa zake kwa umma kila mwezi ili wananchi waweze kufuatilia utekelezaji wa makubaliano.

5. Kutokana na mgogoro huu wa madaktari Serikali ijifunze kuchukuwa  hatua mara moja kila  linapotokea tatizo  ili kuepusha madhara yeyote.

6. Tunawashukuru madaktari kwa kurudi kazini  leo na tumetembelea hospitali zote za umma Mkoani Dar es salaam na tumeshuhudia huduma  za tiba zikiendelea. Tunawaomba sana mwendelee kuwahudumia wananchi kwa moyo wote na linapotokea tatizo meza ya majadiliano itumike ili kuepusha madhara kama tulivyoshuhudia kwenye mgogoro huu

7.Mamlaka zote nchini zitambue,ziheshimu na kuwajibika kwa  wananchi walioziweka madarakani kwa mujibu wa Ibara ya 8 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Pia ni vema tukakumbuka kuwa nchini duniani zimekuwa na tabia ya kuwashikilia.kuwashitaki na kuwatishia watetezi wa haki za binadamu kwa tuhuma zisizo na msingi ili kuendeleza unyanyasaji na ukandamizaji. Serikali itambue kuwa pale Serikali zilipokuwa zikijikita kwenye tabia hizi kandamizi,ziliambulia kuongeza matatizo na hata kuishia kumwaga damu za watu wake na hata viongozi wenyewe. Wanaharakati tunaomba mshikamano na umoja kutoka kwa wananchi wote wenye uchungu na mapenzi mema kwa taifa letu.

Imetolewa na: 
Policy Forum, TGNP, LHRC, SIKIKA, TAMWA, HAKI ARDHI, HAKIELIMU, GDSS, 
Jipange, ForDia, na FemAct.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: