Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki katika Mkoa wa Singida Mheshimiwa Tundu Lissu amelaani kitendo cha Jeshi la Polisi likisaidiwa na viongozi wa Serikali katika Wilaya ya Singida chini ya mkuu wa Wilaya hiyo Paschal Mabiti cha kuwaondoa kwa nguvu maelfu ya wajimbaji wadogo wadogo wa dhahabu na wakazi wa eneo la Taru katika Kata ya Mang'onyi ili kupisha kampuni ya madini ya kigeni Shanta Mining kufanya utafiti wa madini ya dhahabu katika eneo hilo. Wananchi hao waliondolewa katika eneo la kwa mara kwanza kati ya Oktoba na Novemba mwaka jana.
Hata hivyo, wananchi hao walirudi katika eneo hilo wiki ilipita kufuatia walinzi binafsi wa kampuni kuwakamata na baadae kuwapiga na kuwajeruhi wachimbaji na wananchi kadhaa wa eneo hilo. Kitendo hicho kiliwafanya wananchi wenye hasira kuvamia kambi ya Shanta Mining iliyopo katika Kitongoji cha Kinyamberu cha Kijiji cha Mang'onyi kwa lengo la kuwaokoa wananchi wenzao waliokuwa wameumizwa vibaya na walinzi wa kampuni. Siku moja baadae Jeshi la Polisi katika wilaya ya Singida lilimwanga askari polisi wakiwa na silaha nzito ambao waliwakamata na kuwapiga wananchi kadhaa wa Kijiji cha Mang'onyi na baadae kuwaweka rumande kwa kinachodaiwa kuwa ni uvamizi wa kambi ya Shata Mining.
Akizungumzia kitendo cha Jeshi la Polisi cha kuwaondoa kwa nguvu wananchi wa Jimbo lake, Mbunge Lissu ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Katiba na Sheria katika kambi rasmi ya upinzani Bungeni, alisema;"Kwa mara nyingine tena Jeshi la Polisi Tanzania limetumika dhidi ya wananchi ambao kosa lao pekee ni kuzaliwa na kuishi kwenye eneo ambalo lina utajiri wa madini ambao Serikali ya CCM imeamua ukabidhiwe kwa wawekezaji wa kigeni badala ya kuwasaidia wananchi wake. Kwa mara ya nyingine tena Jeshi la Polisi limethibitisha kwamba Jeshi hilo ni mkono wa mabavu wa makampuni ya madini ambao unatumika kuwanyang'anya wananchi wazawa utajiri wao wa asili na kuukabidhi kwa makampuni tajiri ya kigeni kwa kisingizio cha uwekezaji"
Akifafanua jambo hilo, Mbunge Lissu alisema; "Hii siyo mara ya kwanza kwa Jeshi la Polisi Tanzania kutumika ama wakala wa kibavu wa makampuni ya madini ya nje. Watanzania hawajasahau jinsi Jeshi hilo lilivyotumika kuwaondoa maelfu ya wachimbaji wadogo wadogo wa dhahabu wa Bulyanhulu wilaya Kahama katika mkoa wa Shinyanga kati ya Julai na Agosti 1996, kitendo kilichopelekea wachimbaji wengi kuuawa kwa kufukiwa kwenye mashimo ya dhahabu wakiwa hai. Na wala hatujasahau jinsi Jeshi la Polisi Tanzania lilivyowaondoa kwa nguvu wachimba wadogo wadogo wa eneo la Lissu wilayani Nzega ili kupisha makampuni ya Ki-Australia kuchimba dhahabu katika eneo hilo Septemba 1996. Aidha, bado tuna kumbukumbu za jeshi la Polisi kuwaondoa wananchi wa Nyamongo katika wilaya ya Tarime na kuwapa Wa-Australia wengine mgodi wa Dhahabu wa North mara mwezi Agosti 2001, kitendoambacho kimesababisha watu wengi wa maeneo ya Nyamongo kupoteza maisha yao kutokana na kuuwa na Jeshi la Polisi au kutokana na sumu na kemikali zinazozalishwa na mgodi huo.
Mheshimiwa Lissu alilitaka Jeshi la Polisi Tanzania kudhibitisha kwamba ni Jeshi la Polisi la Watanzania badala ya kutumikia maslahi ya kiuchumi ya makampuni ya madini ya nje kwa kuacha mara moja vitendo vya kutumia nguvu za silaha dhidi ya wananchi wanaotaka kutumia rasilimali za maeneo yao kujipatia riziki na kukimu maisha yao na watoto wao. Aidha, aliutaka uongozi wa ngazi za juu wa Jeshi la Polisi kuwachukia hatua viongozi wa Jeshi la Polisi hilo katika wilaya ya Singida kwa kutumia nguvu kuwaondoa wananchi kwenye maeneo yao wakati kesi iliyofunguliwa na wananchi hao dhidi ya makampuni ya Shata Mining mwaka 2009 ikiwa bado haijatolewa uamuzi na Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Ardhi. "Tangu mwaka 2009, wananchi 18 wa maeneo ya Taru na Mang'onyi wamefunguka Keshi ya Ardhi Na. 21 ya 2009 dhidi ya Shanta Mining kwa kutwaa kwa nguvu maeneo yao ya Kilimo na Makazi. Wakati Mahakama Kuu haijatoa uamuzi juu ya kesi hiyo, tayari Jeshi la Polisi Tanzania limetumika kuimilikisha Shanta Mining maeneo hayo kwa nguvu na kinyume cha sheria kwa kuwaondoa wananchi wa Taru na Mang'onyi kutoka kwenye ardhi zao. Sasa Mahakama Kuu itakabiliwa na fait accomplish kwani uamuzi wowote itakaoutaka kwenye keshi hiyo utaikuta Shanta Mining ikiwa inashikilia na kutumia eneo hilo. Utamaduni huu wa Jeshi la Polisi kutumia nguvu wakati masuala yenye utata yako mahakama hauna budi kulaaniwa na kupingwa na watu wote wanaoheshimu utawala wa sheria katika nchi yetu".
Wakati huo huo Mbunge amemtaka waziri wa Nishati na Madini William Ngeleja kutimiza ahadi aliyowapa wananchi wa Kata ya Mang'onyi kwamba Wizara yake itawatengea eneo la Taru kwa ajili ya uchimbaji wao badala kulingawa kwa Shanta Mining. "Mheshimiwa Ngeleja alituahidi mimi pamoja na ujumbe wa mamancho wa vijiji vya Sambaru na Mang'onyi waliokuja kumwona Bungeni mwaka jana kwamba eneo la Taru lingetengwa kwa ajili ya wachimbaji wadogo wadogo wa dhahabu. Badala ya kutimiza ahadi yake kwa wananchi Waziri Ngeleja amefanya kama alivyofanya Dk. William Shija aliyemrithi kiti cha Ubunge wa Sengerema na mikoba ya uwaziri wa Nishati na Madini kwa kuamuru kuondolewa kwa wachimbaji wa Bulyanhulu. Matendo ya aina hii ndiyo yanayompunguzia Waziri huyu heshima kwa Watanzania na ndiyo maana kamati ya Bunge ilichunguza kashfa ya Jairo mwaka jana ilipendeleza Waziri Ngeleja ajiuzuli au aondolewe uwaziri.
Shanta Mining ni kampuni tanzu ya Shanta Gold Ltd, kampuni ya kugeni iliyosajiliwa katika visiwa vya Guernsey nchini Uingereza. Shanta Gold imesajiliwa katika soko Mbadala la hisa la London, Uingereza (AIM) na zaidi asilimia 50 ya hisa zake zinamilikiwa na wawekezaji kutoka Uingereza, Uswisi na Canada. Uraia wa wenye hisa wengine haujulikani laini Mahesh Patel na Ketan Patel ambao ni wenye hisa wengine wanatajwa kuwa ni wakazi wa Tanzania na Kenya.
Tangu ilipopewa leseni ya utafiti wa dhahabu kwenye maeneo ya Kata ya Mang'onyi, kampuni ya Shanta Mining imekuwa na mgogoro mkubwa na wamilikiwa ardhi wa maeneo hayo. Mwaka 2006 kampuni hiyo pamoja na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Singida wakati huo Kapteni James Yamungu, aliyekuwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya Vicent Shilogile na viongozi wa kadhaa wa Kata na Kijiji walishtakiwa na wakazi watano wa kijiji cha Mang'onyi kwa madai ya kulitumia Jeshi la Polisi kuwakamata na baadae kuwafungia mashtaka ya kufanya mkutano haramu ambayo hata hivyo walifutwa badala ya kukosekana ushahidi. Katika kesi zote hizi Mheshimiwa Lissu amekuwa pia wakili wa wananchi ambao wameathiriwa na kuondolewa kwa lesseni ya utafiti kwa Shanta Mining.
Toa Maoni Yako:
0 comments: