*Picha za Video zaonyeshwa mkutanoni na kuwaumbua Askari watenda makosa
Na Mwandishi wa Jeshi la Polisi –Zanzibar
ZANZIBAR IJUMAA JANUARI 27, 2012. Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama Zanzibar, wamekutana na kujadili masuala mbalimbali ya kiusalama na kutilia mkazo suala la utii wa sheria bila shuruti kwa maafisa na askari wa vyombo hivyo.
Afisa Habari wa Jeshi la Polisi Zanzibar Inspekta Mohammed Mhina, amesema kuwa pamoja na mambo mengine maafisa hao pia wamekubaliana kuwasimamia kwa karibu waliochini yao ili kuepuka kufanya vindendo viovu vikiwemo vya uvunjifu wa sheria mbele za raia.
Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wake ambaye pia ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Zanzibar ACP Aziz Juma Mohammed, amesema kuwa watumishi wa vyombo vya ulinzi na usalama ni miongoni mwa watu muhimu wanaopashwa kutii sheria ili kuonyesha mfano kwa mwananchi.
Kamanda Aziz amesema kuwa pamoja na kutolewa kwa amri ya uvaaji wa kofia ngumu kwa askari wanapoendesha pikpiki lakini baadhi ya maafisa na askari wamekuwa wakikaidi amri hiyo ambayo pia ni sehemu ya sheria mama na kuendelea kuendesha vyombo hivyo bila ya kuwa na kofia za kujikinga na ajali.
“Tukienda mbele, huko tunaweza tukajikuta kwamba sisi ni sehemu kubwa ya watu ambao hatutii sheria ingawa tulitegemewa sana tusimamie sheria lakini kinyume chake sisi tunaangukia kwenye kundi la wale ambao wasiotii sheria”. Alisema Kamanda Aziz.
Katika mkutano huo, Makamanda hao walionyeshwa picha za video za askari waliochini yao kutoka majeshi na vikosi vyote vya Ulinzi na Usalama Visiwani Zanzibar wakiwa wanavunja sheria mbalimbali zikiwemo za kuendesha pikipiki huku wakiwa na sare za kazi bila ya kufuata sheria na taratibu za usalama barabarani.
Naye Mkuu wa Rada za KMKM Kamanda CDR Mohammed Mussa Seifu, amesema kuwa amri ilishatoka kuwa ni marufuku kwa Askari wa Jeshi ama Kikosi chochote kuonekana akiendesha pikipiki bila ya kuvaa kofia ngumu za kujikinga na ajali.
Amesema katika hilo kama mtu atakamatwa hakuna kiongozi atakayejitokeza kumsaidia mtu huyo na hivyo ni kazi ya Askari wa Usalama barabarani kuhakikisha kuwa wanamchukulia hatua mtu yeyote atakayevunja sheria ya usalama barabarani bila kujali kama ni askari ama Raia wa kawaida.
Kwa upande wake Mkuu wa Polisi Viwanja vya Ndege Zanzibar ASP Omari Khamis Abdallah na Luten Kamanda wa KMKM LCDR Khamis Khamis, wamewataka askari wa usalama barabarani kuanza kuwachukulia hatua kali wenzao wanaovunja sheria ili kuonyesha utii wa sheria za nchi mbele ya raia na kuonyesha mfano.
Wametaka kila kiongozi sehemu ya kazi kuhakikisha kuwa waliochini yake wanafuata sheria na taratibu sio tu za usalama barabarani bali pia na kuzingatia na kusimamia sheria mbalimbali ili iwe rahisi kumkamata na kumchukulia hatua raia wa kawaida.
Mbali ya Vikao vya kawaida vya Ulinzi na Usalama, Viongozi hao pia wameazimia kukutana kila baada ya miezi mitatu ili kujadili na kuyapatia ufumbuzi mambo mbalimbali zikiwemo kero na mataizo yanayojitokeza kwao na kwa watendaji waliochini yao.
Mkutano huo ambao umefanyika Makao Mkuu ya Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, pia umehudhuriwa na Maafisa kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jeshi la Polisi, Uhamiaji, Usalama wa Taifa, Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) Kikosi cha Kuzuia Magendo (KMKM), Kikosi cha Valantia (KVZ), Mafunzo (MF)na Zimamoto na Uokoaji (KZU).
Toa Maoni Yako:
0 comments: