Spika wa Bunge, Anne Makinda, akitoa wasifu wa mare hemu katika shughuli zake za kibunge na salam za rambirambi kwa niaba ya Bunge.
---
SPIKA wa Bunge la Tanzania, Mhe. Anne Makinda amesema aliyekuwa Mbunge wa Viti wa Maalum mkoa wa Morogoro (CHADEMA) Bi. Regia Mtema ni nyota inayong’aa kwani ameweza kuwaunganisha Watanzania wote bila kujali tofauti za kiitikadi zilizopo katika jamii.
Ametoa kauli hiyo leo asubuhi (Jumanne, Januari 17, 2012) wakati akitoa salamu za rambirambi wakati wa kuuaga mwili wa Mhe. Regia Mtema kwenye viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam kabla ya kusafirishwa kwenda Ifakara kwa mazishi. Bi. Mtema alifariki Jumamosi, Januari 14, mwaka huu kwa ajali ya gari iliyotokea eneo la Ruvu, mkoani Pwani.
“Regia ni nyota inayong’aa, ametuunganisha Watanzania kupitia upendo aliokuwa nao… ametuonesha kuwa hizi itikadi ni za kupita tu,” alisema huku akishangiliwa na mamia ya waombolezaji waliofurika katika viwanja hivyo wakiwemo viongozi wa kitaifa, mawaziri, wabunge na wananchi wa kawaida.
Akizungumzia kuhusu utendaji kazi wa marehemu Mtema, Spika Makinda alisema alimfahamu mapema wakati (yeye) akiwa Mwenyekiti wa Wabunge wanawake kupitia mafunzo waliyokuwa wakitoa kwa vijana kama njia ya kuhamasisha wanawake wagombee majimboni na hivyo kuongeza idadi ya wabunge wanawake.
“Regia ni mfano kwa wanawake wengi kwa sababu alithubutu kugombea jimbo licha ya vikwazo vilivyopo ambavyo huwafanya wanawake wengi waogope kugombea majimboni…, nawasihi wanawake wote muige mfano wake,” alisisitiza.
“Regia alikuwa na nyumba aliyoinunua kule Mbezi na alikuwa akiishi na watu wengi wenye matatizo, hakuwa na kazi ya maana, hakuwa na mshahara mkubwa lakini alithubutu kuwasaidia wenye matatizo. Regia ametupa fundisho, ni mtoto lakini pia ni mfano wa kuigwa na wabunge wote,” aliongeza Mama Makinda.
Mapema akitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya Serikali, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisema ataendelea kumkumbuka Mhe. Regia kwa sababu alikuwa kiungo kizuri Bungeni na aliisadia Serikali kupata maoni ya wananchi kwa haraka zaidi.
“Mhe. Regia ni kiongozi ambaye ataendelea kukumbukwa kwa sababu ya mchango wake… nimeongea na Mhe. Mbowe na kumwambia kwamba pengo la Regia mtaliziba lakini hamtapata mtu wa kufanana naye kwa sababu Regia alikuwa na karama za pekee”.
Alitoa pole kwa Chama cha Maendelea na Demokrasia (CHADEMA) kwa kumpoteza mbunge mahiri na makini. Pia alitoa pole kwa wazazi na familia na kuwasihi wajipe moyo na kufarijiana. Aliwaomba wajiombee pia ili waweze kukabili majonzi ya msiba huo na akawataka waendeleze mshikamano kama familia.
Alisema Watanzania kama jamii, kila mmoja ana jukumu la kuendeleza yale mazuri ambayo Mhe. Regia alikuwa akiyasimamia.
Viongozi wengine waliotoa salamu za rambirambi ni Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Wilboad Slaa na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Mhe. Freeman Mbowe ambao waote walielezea ushiriki wa Mhe. Regia katika nafasi za uongozi tangu mwaka 2005 alipojiunga na chama hicho.
Shughuli ya kuuaga mwili wa Mhe. Regia Mtema iliongozwa na Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal.
Mbali ya Kamati ya Uongozi ya Bunge na Kamati ya Huduma za Bunge, wabunge wengine watakaoshiriki mazishi ya Mhe. Regia Mtema huko Ifakara hapo kesho (Jumatano, Januari 18, 2012) ni wabunge wote wa mkoa wa Morogoro na wabunge 10 kutoka Kamati ya Miundombinu ambayo Mhe. Regia alikuwa mjumbe.
Wengine ni wabunge sita kutoka (CCM), wabunge wanne (CUF), mbunge mmoja mmoja kutoka NCCR, TLP, UDP na chama cha wabunge wanawake.
Serikali itawakilishwa katika mazishi hayo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utumishi), Bi. Hawa Ghasia.
Toa Maoni Yako:
0 comments: