Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Mheshimiwa Freeman Mbowe, kuomboleza kifo cha Mbunge wa Viti Maalum wa chama hicho, Mheshimiwa Regina Mtema.
Mheshimiwa Mtema ambaye pia alikuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema na Waziri Kivuli wa Kazi na Ajira amefariki dunia katika ajali ya gari iliyotokea maeneo ya Ruvu, Mkoa wa Pwani, asubuhi ya leo Jumamosi, Januari 14, 2012.
Katika salamu zake, Mheshimiwa Rais Kikwete amemwambia Mheshimiwa Mbowe kuwa amesikitishwa na kuhuzunishwa na habari za kifo cha mbunge huyo ambaye amepoteza maisha akiwa bado kijana na kwamba pigo hilo siyo kwa Chama cha Chadema peke yake bali ni kwa taifa zima.
“Nimepokea kwa masikitiko na huzuni nyingi habari za kifo cha Mheshimiwa Mtema katika ajali ya gari. Siyo kwamba ajali hii imechukua maisha ya kijana bali imelinyang’anya taifa mbunge hodari, na kwa hakika, kifo chake siyo tu ni pigo kwa chama chako cha CHADEMA bali ni pigo kwa sote na kwa taifa letu kwa jumla. Nakutumia wewe binafsi, chama chako na wanachama wake salamu za dhati ya moyo wangu kuomboleza kifo na msiba huu mkubwa.”
“Napenda ujue kuwa niko nanyi katika msiba huu. Napenda vile vile uniwasilishie salamu zangu za rambirambi za dhati kabisa kwa wana-familia, ndugu na jamaa wa marehemu Mheshimiwa Mtema. Wajulishe kuwa nimepokea habari hizo kwa uchungu mwingi na kuwa moyo wangu uko nao katika wakati huu mgumu wa maombolezo, “ amesema Mheshimiwa Rais na kuongeza.
“Aidha, wajulishe kuwa nawaombea kwa Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, awajalie uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu kwa sababu yote ni mapenzi yake. Naungana nawe, Mheshimiwa Mwenyekiti, na wanafamilia wa marehemu kumwomba Mwenyezi Mungu aiweke pema peponi roho ya Mheshimiwa Regina Mtema. Amen.”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu,
DAR ES SALAAM.
14 Januari, 2012
Toa Maoni Yako:
0 comments: