Na Mohammed Mhina, Handeni
Wananchi
wa Wilaya ya Handeni Mkoani Tanga, wamepongeza juhudi zinazochukuliwa
na Jeshi la Polisi mkoani humo katika kukabiliana na uhalifu wa utekaji
wa magari na makosa ya usalama barabarani.
Wakizungumza
katika kikao cha maendeleo ya Kijiji cha Makanya, Mzeri wilayani
Handeni, wananchi hao wamesema kuwa uhalifu wa utekaji wa magari na
kuporwa mali za abiria uliokuwepo siku za nyuma wilayani Handeni hivi
sasa vimekoma kabisa kutokana na kuimarishwa kwa doria hizo za
barabarani.
Mzee
Hussein Ramadhani, amesema kuwa kuimarishwa kwa doria hizo, pia
kumepunguza matukio ya ajali za barabarani zikiwemo zile
zinazosababishwa na uendeshaji wa pikipiki maarufu kama bodaboda bila ya
leseni ama kuvaa kofia ngumu za kujikinga na ajali.
Wananchi
hao wamesema mikakati ya pamoja inayochukuliwa na Kamanda wa Polisi
mkoa wa Tanga ACP Costantino Masawe na Mkuu wa Upelelezi wa mkoa huo SSP
Jaffari Mohammed zimewezesha hali ya wilaya ya Handeni na mkoa mzima wa
Tanga kuwa shwari.
Wamesema
juhudi za pamoja zinazofanywa na Mkuu wa Polisi wa wilaya ya Handeni
SSP Seith Mwakajinga, Mkuu wa Upelelezi SP Aziz Kimata na Mkuu wa Kituo
cha Polisi Handeni ASP Peter Ngoro, zimepelekea kuimarika kwa hali ya
Ulinzi na Usalama wilayani humo.
Naye
Mzee Mwinjuma Rashidi Tilibwinda, amewataka Polisi kutowaoenea haya
wale wote wanaoendesha pikipiki na kubeba abiria huku wakiwa hawana
leseni za udereva ama kuvaa kofia ngumu vichwani za kuwakinga na madhara
wapatwapo na ajali ili kupunguza ajali za barabarani zitokanazo na
uendeshaji mbaya wa pikipiki.
Amesema
kuwa mara nyingi wanaoendesha pikipiki hizo ni vijana wadogo ambao
uwezo wao wa kufikiri na kuchukua tahadhari za kujiepusha na ajali ni
mdogo.
Pamoja
na pongezi hizo, za kuwadhibiti wapanda pikipiki, lakini Mzee
Tilibwinga amependekeza kuwepo na elimu juu ya matumizi salama ya vyombo
vya moto kwa vijana hao kwa lengo la kuwaepushia na matukio ya ajali za
barabarani.
Wamesema
kama mikoa mingine ingeweza kuiga mfano huo, ni wazi kuwa uhalifu na
ajali za barabarani hapa nchini ungeweza kukoma kabisa.
Kwa
upande wake Kamanda wa Polisi Mkoani Tanga ACP Costantino Masawe,
amesema kuwa Jeshi la Polisi mkoani humo litaendelea kuimarisha doria
katika barabara mbalimbali ili kuwahakikishia wananchi usalama wao.
hata
hivyo Kamanda Masawe ametoa wito wananchi wanaoishi kandokando mwa
barabara kuu mkoani humo, kutoa taarifa Polisi wanapoona dalili za
kuwepo kwa vitendo vya kihalifu vikiwemo vya madereva kuendesha mwendo
wa kasi ili kunusuru abiria hasa katika kipindi hiki cha kuelekea siku
kuu za mwisho wa mwaka.
Toa Maoni Yako:
0 comments: