Tarehe 31 Desemba, 2010, Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt.
Jakaya Mrisho Kikwete katika salamu zake za mwaka mpya wa 2011 kwa
Watanzania, kati ya masuala aliyozungumzia ni pamoja na kuliarifu Taifa kuhusu
Maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara yatakayofanyika mwaka 2011
ambapo yatafanyika nchi nzima na kilele chake kuwa tarehe 9 Desemba, 2011.
Maadhimisho ya Miaka 50 ya Uhuru yalizinduliwa
rasmi tarehe 1 Juni, 2011 Mjini Songea na Makamu wa Rais Mheshimiwa Dkt. Mohamed
Gharib Bilal. Mambo mbalimbali yamefanyika hadi sasa na maandalizi yanaendelea
ili kuhakikisha kwamba Maadhimisho hayo yanafanyika kwa ufanisi na uzito
unaostahili.
(i)
Ratiba ya Maadhimisho kwa Wizara, Mikoa na Sekta Binafsi:
Wizara, Mikoa na Sekta Binafsi zimefanya
maonesho ya kuelezea mafanikio yaliyopatikana katika Nyanja mbalimbali katika
kipindi cha Miaka 50 ya Uhuru kama ilivyopangwa. Ratiba imekamilika jana tarehe 30 Novemba,
2011.
(ii)
Taarifa za Miaka 50 ya Uhuru za Wizara na
Mikoa
Wizara/Mikoa imeandaa taarifa za Mafanikio
ya Miaka 50 ya Uhuru. Taarifa hizo
pamoja na kutumiwa na Wizara/Mikoa wakati wa Maadhimisho ya ratiba zao,
zimetumika pia katika kuandaa Taarifa Jumuishi ya Kitaifa.
Taarifa hizo zimewekwa kwenye Tovuti ya Taifa, Tovuti ya Ofisi ya
Waziri Mkuu na Tovuti maalum iliyoanzishwa kwa ajili ya Maadhimisho haya.
(iii)
Taarifa Jumuishi ya Kitaifa ya Miaka
50 ya Uhuru
Taarifa Jumuishi ya Kitaifa ya Miaka
50 ya Uhuru imeandaliwa na kuchapishwa kwa Kiswahili na Kiingereza. Taarifa hiyo watagawiwa Wananchi na Wadau
wengine.
(iv)
Kutangaza Mafanikio Yaliyopatikana
katika Vyombo vya Habari vya Ndani na Nje ya Nchi:
(a)
Vyombo vya Habari vya Nje ya Nchi
Makala zimeandaliwa na zitatolewa
katika Vyombo vya Habari mbalimbali vya nje na kusambazwa katika maeneo mbalimbali. Vyombo
vya Habari vitakavyotumika ni pamoja na:
- The New African Magazine (Uingereza);
- World Report (Gazeti la Independent la Uingereza); na
- Asia Business Channel Television.
(b) Vyombo vya Habari vya Ndani
Makala mbalimbali zimeandaliwa kuhusu
Mafanikio yaliyopatikana katika Miaka 50 ya Uhuru. Makala hizo zitatolewa kwenye vyombo vya
habari vya ndani.
(v)
Tovuti ya Maadhimisho ya Miaka 50 ya
Uhuru
Katika kufanikisha Maadhimisho haya na
kuhakikisha taarifa mbalimbali kuhusu
Maadhimisho ya Miaka 50 ya Uhuru zinaufikia Umma, Tovuti maalum ya Maadhimisho
ya Miaka 50 ya Uhuru imeanzishwa (www.tanzania50uhuru.go.tz).
Aidha, tovuti ya Taifa (www.tanzania.go.tz) na ya
Ofisi ya Waziri Mkuu (www.pmo.go.tz) zinatumika pia katika kutoa
habari za Maadhimisho haya.
Ili kuhakikisha usahihi wa Taarifa zinazowekwa
katika Tovuti ya Miaka 50 ya Uhuru kimeanzishwa kituo cha kutolea habari za
Miaka 50 ya Uhuru katika Idara ya Habari (MAELEZO).
(vi)
Mialiko ya Viongozi kutoka Nje ya
Nchi
Mhe. Rais amealika Viongozi kutoka
Nje ya Nchi zikiwemo Nchi za SADC na Afrika Mashariki kujumuika nasi katika
kusherehekea Miaka 50 ya Uhuru. Tayari Ma-Rais
wa Nchi Nane (8), Makamu wa Rais wa Nchi Tatu (3), Mawaziri Wakuu wa Nchi Tatu
(3) pamoja na Viongozi Wawakilishi 16 wamethibitisha kuhudhuria Maadhimisho
haya.
(vii)
Mialiko ya Viongozi wa Ndani ya Nchi
Viongozi wa Kitaifa waliopo
madarakani na Wastaafu, na wa Vyama vya Siasa (Wenyeviti na Makatibu Wakuu)
wamepelekewa mialiko ya kuhudhuria Sherehe hizo na wengi wao wamethibitisha
kuhudhuria Maadhimisho haya.
(viii)
Mialiko Maalum ya Mhe. Rais ya Viongozi wa Ndani ya Nchi
Mhe. Rais ametoa mialiko maalum kwa Wajumbe wote
wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Wazee Mashuhuri kutoka Mikoa mbalimbali, baadhi ya
Wenyeviti na Makatibu wa Chama Tawala kutoka Mikoa mbalimbali.
(ix)
Mbio za Mwenge wa Uhuru Mwaka 2011
Mbio za Mwenge wa
Uhuru mwaka 2011 zimetumika pia kama sehemu ya Maadhimisho ya Miaka 50 ya Uhuru
katika kuelezea mafanikio ya Serikali.
Mwenge uliwashwa rasmi na Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Mohamed Gharib Bilal katika kijiji cha
Butiama tarehe 14 Oktoba, 2011.
Ujumbe wa Mbio za
Mwenge wa Uhuru mwaka huu ni “Miaka 50
ya Uhuru: Tumethubutu, Tumeweza na
Tunazidi Kusonga Mbele”. Aidha,
Mapambano dhidi ya Ugonjwa wa UKIMWI, Dawa za Kulevya na Rushwa ni sehemu ya
Ujumbe huo.
Sherehe za kilele cha Mbio
za Mwenge wa Uhuru zinafanyika leo tarehe 1 Desemba, 2011 huko Dar es
Salaam. Mgeni Rasmi katika Sherehe hiyo
atakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho
Kikwete ambaye atapokea Mwenge huo katika Uwanja wa Uhuru na kuwakabidhi Wanajeshi
watakaoupandisha katika Mlima Kilimanjaro.
(x)
Wiki ya Maonesho ya Maadhimisho ya Miaka
50 ya Uhuru (Tarehe 1 - 12 Desemba, 2011)
Kutakuwa na Wiki ya Maonesho ya Maadhimisho
haya katika Viwanja vya Mwalimu J. K. Nyerere ambayo yameanza leo tarehe 1 - 12
Desemba, 2011. Wizara na Mikoa, Sekta
Binafsi na Wafanyabiashara mbalimbali wa Kimataifa na Ndani ya Nchi watashiriki
katika Maonesho hayo ambayo hayatakuwa na kiingilio. Maonesho hayo yatafunguliwa na Mheshimiwa
Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi tarehe
2 Desemba, 2011 katika Viwanja vya Mwalimu J. K. Nyerere.
Utaratibu
umewekwa kwa Viongozi wa Kitaifa waliopo Madarakani na Wastaafu wamealikwa
kutembelea Maonesho haya. Aidha, Mikoa
yote itafanya Maonesho kama haya katika ngazi ya Mikoa na wageni rasmi watakuwa
Wakuu wa Mikoa husika. Wananchi wanaombwa kujitokeza kwa wingi kwenye Maonesho hayo.
(xi)
Mkesha wa Uhuru Usiku wa Tarehe
8/12/2011
Kutakuwa na Sherehe za Mkesha wa Uhuru katika
Viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam usiku wa tarehe 8/12/2011 kuamkia tarehe
9/12/2011. Katika Sherehe za Mkesha huo Burudani mbalimbali zitakuwepo na
shughuli kubwa itakuwa ni urushaji wa fashifashi (fireworks) ambazo zitarushwa Saa 6.01 usiku.
Kutakuwa pia na shughuli za Mkesha usiku huo
wa tarehe 8/9/2011 katika Manispaa zote za Dar es Salaam, ikiwemo Kinondoni (Viwanja
vya Kawe) na Temeke (Viwanja vya Zakhem). Shughuli kubwa usiku huo itakuwa ni Burudani na
Urushaji wa Fashifashi.
(xii)
Maadhimisho ya Siku ya Kilele tarehe
9 Desemba, 2011
Sherehe za Kilele zitafanyika katika Uwanja
wa Uhuru, Dar es Salaam tarehe 9/12/2011. Mgeni rasmi katika Sherehe hizo atakuwa Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete.
Pamoja na shughuli mbalimbali
zitakazofanyika siku hiyo kutakuwa na:
· Gwaride
Vikosi ya Ulinzi na Usalama kwa
pamoja vimeandaa Gwaride la Miaka 50 ya Uhuru.
Kutakuwa na Onesho la Zana mbalimbali za Kivita.
·Halaiki
Imeandaliwa Halaiki ya Wanafunzi wa Shule
za Msingi wapatao 4,550 na Wanafunzi wa Shule za Sekondari wa uhamasishaji
wapatao 2,000.
·Ngoma za Asili
Kutakuwa na Vikundi vya Burudani kutoka
Dar es Salaam vitakavyotumbuiza. Aidha, vimeandaliwa vikundi vinne kutoka Mikoa
mitatu Nchini pamoja na Zanzibar ambavyo vitatumbuiza. Vikundi hivyo ni:
- Ngoma
ya Ngongoti kutoka Mtwara;
- Ngoma
ya Selo kutoka Pwani;
- Ngoma
ya Bugobogobo kutoka Mwanza; na
- Ngoma
ya Msewe kutoka Zanzibar.
Ninawaomba wananchi wote kwa ujumla waliopo
Dar es Salaam na Mikoani kujitokeza kwa wingi kusherehekea Miaka 50 ya Uhuru wa
Nchi yetu.
“Tumethubutu, Tumeweza, Tunazidi
Kusonga Mbele”.
Mizengo P. Pinda (Mb.)
WAZIRI MKUU
01 Desemba 2011
Toa Maoni Yako:
0 comments: