YAH: UFAFANUZI KUHUSU HABARI YA GAZETI LA TANZANIA DAIMA LA
TAREHE 5/9/2011 ILIYOSEMA “UCHUNGUZI UDA KUANZA LEO”


Katika Gazeti la Tanzania Daima la tarehe 5 Septemba 2011 lilichapisha habari yenye kichwa kilichosomeka “Uchunguzi UDA kuanza leo” ikieleza kuwa kamati iliyoundwa na Bunge kuchunguza kashfa ya uuzwaji wa Shirika la Usafiri Dar es salaam (UDA) ilitarajia kuanza kazi yake siku ya Jumatatu 5 Septemba 2011 chini ya uwenyekiti wa Mhe. Murtaza Mangungu, Mbunge wa Kilwa Kaskazini CCM.

Ofisi ya Bunge inapenda kutoa taarifa kwa vyombo vya Habari na Umma kwa ujumla kuwa taarifa hiyo ni potofu na haina ukweli wowote. Ukweli ni kwamba mpaka sasa hakuna kamati yoyote ya Bunge inayochunguza suala la uuzwaji wa Shirika la Usafiri Dar es salaam (UDA). 

Ikumbukwe kwamba wakati wa Bunge la Bajeti, Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Mashirika ya
Umma Mhe. Zitto Kabwe (Mb) aliongea na waandishi wa Habari kuhusu nia ya Kamati yake kufanya uchunguzi huo ikiwa ni pamoja na mapendekezo ya wajumbe aliyowasilisha kwa Mhe. Spika kwa lengo la kupata kibali chake kwa muibu wa Kanuni za Bunge.

Aidha, ifahamike kuwa uamuzi wa Mhe. Spika kuhusu suala hilo ulikuwa ni kuliacha lichunguzwe na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za serikali (CAG) na baadae CAG awasilishe taarifa ya uchunguzi wake Serikalini na hatimaye Bunge liarifiwe matokeo ya Uchunguzi huo kupitia Serikali.

Hata hivyo ieleweke kuwa, Kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la 2007, Kanuni ya 117, inaeleza kuwa Bunge linaweza kuunda Kamati Teule kwa madhumuni maalumu kwa hoja Mahususi itakayotolewa na Kuafikiwa Bungeni.

Na fasili ya (4) inasema kuwa wajumbe wa kamati Teule watateuliwa na Spika na watamchagua Mwenyekiti wa Kamati hiyo kutoka miongoni mwao. Pili, kanuni ya 114 (3) inatamka bayana kuwa kamati ya kudumu itakutana kila inapoitwa na Spika, Naibu Spika au na Mwenyekiti wake baada ya kupata idhini ya Spika.

Mwandishi wa habari hiyo, hakufuatilia uhalali wa kile alichokusudia kuandika na hata kujiridhisha na utaratibu wa kamati zinavyofanya kazi kwa mujibu wa kanuni na badala yake aliandika maoni yake kwa jinsi alivyohisi. Hili ni jambo la hatari!

Mwisho, tunapenda kuwakumbusha waandishi wote wa Habari kuzingatia miiko ya kazi yao na kuwa makini waandikapo jambo lolote kwa wasomaji wao, kwani wasipofanya hivyo na kuandika habari za kupotosha, wanasababisha usumbufu usio wa lazima na wanaweza kulaumiwa kusababisha mikanganyiko miongoni mwa jamii yetu.

Ofisi ya Bunge inapenda kuwaarifu wananchi wote wakiwemo wanahabari kuwa Idara yake ya Habari imekuwa ikitoa na itaendelea kutoa ushirikiano wa kutosha kuwaarifu waandishi kuhusu taarifa zozote wanazohitaji na hususani wanazotaka kuandikia habari.

Aidha, tunasikitishwa na uandishi wa namna hii wa kuandika kwa kutegemea hisia bila hata kufanya jitihada za kutosha za kuwasiliana na Ofisi ya Bunge.

Ofisi ya Bunge iko wazi kutoa ushirikiano kwa ufafanuzi wowote utakaohitajika.

Imetolewa na:
Idara ya Habari, Elimu kwa Umma na Uhusiano wa Kimataifa
Ofisi ndogo ya Bunge
Dar Es Salaam
8 Septemba 2011.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: