WAREMBO 30 kutoka kanda mbalimbali hapa nchini Septemba 10, 2011 wanatarajiwa kupanda jukwaani kwenye ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam, katika fainali za shindano la kuwania taji la Vodacom Miss Tanzania, 2011.

Warembo hao ambao wamekuwa kambini kwa wiki kadhaa sasa, wakianzia katika hoteli ya Giraffe, jijini Dar es Salaam na baadaye kwenye jumba maalum lililojulikana kama ‘Vodacom House,’ watakuwa katika mchuano mkali wa kumrithi mrembo wa mwaka jana, Genevieve Emmanuel Mpangala, ambaye atalivua taji.

Chini ya udhamini wa kampuni ya simu za mikononi ya Vodacom, warembo hao wakiwa kambini walipata kujifunza masuala kadhaa ya kijamii, sambamba na kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii nchini na kufanya shughuli za kijamii.

Kama ilivyo ada, mashindano hayo kila mwaka huwa na upinzani mkali, ukihusisha kanda kutokana na kila eneo kuwa limejipanga vema kwa kutafuta warembo wenye sifa na vigezo vinavyostahili ili kuhakikisha wananyakua taji.

Wakati taji hilo likiwa linashikiliwa na Kanda ya Temeke, lakini Kanda za Ilala, Kinondoni, Nyanda za Juu Kusini, Ziwa, Kaskazini, Elimu ya Juu, Kati na Mashariki, nazo zimepania mwaka huu kuhakikisha zinatwaa taji hilo.

Hata hivyo, kabla ya fainali zinazolindima leo, kulifanyika mashindano ya kuwania mataji madogo yaliyofanyika kwa nyakati tofauti, ambako washindi wake walikata tiketi ya kutinga moja kwa moja hatua ya nusu fainali ya shindano hilo, ambayo itahusisha warembo 15 badala ya 10 kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.

Warembo ambao tayari wametinga nusu fainali na mataji yao kwenye mabano ni pamoja na Mwajabu Juma (Top Model), Rose Albert (Talent), Tracy Mabula (Miss Photogenic),  Loveness Flavian (Top Sports Woman) na Alexia William (Miss Personality).

Mbali na warembo hao, washiriki wengine wa shindano hilo ni pamoja na Chiaru Masonobo, Zerulia Manoko, Maua Kimambo, Dalilah Ghalib, Christine Mwenegoha, Chritine William, Atu Daniel, Leyla Juma, Zubeda Seif, Stacey Alfred, Husna Twalib, Cynthia Kimasha, Neema Mtitu, Weirungu David, Glory Lory, Blessing Ngowi, Asha Salehe, Mariaclara Mathayo, Irene Karugaba, Glory Samwel, Stella Mbuge, Husna Maulid, Hamisa Hussein, Salha Israel na Jenifer Kakolaki.

Aidha, mshindi katika shindano hilo atazawadiwa gari jipya aina ya Jeep Patriot, lenye thamani ya sh milioni 72, pamoja na fedha taslim milioni 8, huku mshindi wa pili atajitwalia fedha taslim shilingi milioni 6.2, wakati wa tatu atapata shilingi milioni 4.

Mshindi wa nne, ataondoka na shilingi milioni 3, wa tano atapata shilingi milioni 2.4, wakati wa sita hadi wa 15 kila mmoja atapata milioni 2. Mshindi wa 16 – 30, kila mmoja atapata kifuta jasho cha shilingi 700,000.

Tangu kuanza kwa shindano hili mwaka 1994, taji lilinyakuliwa na Aina Maeda, Emily Adolf (1995), Shose Sinare (1996), Saida Kessy (1997), Basila Mwanukuzi (1998), Hoyce Temu (1999), Jacquiline Ntuyabaliwe (2000), Happiness Magese (2001), Angela Damas (2002), Sylvia Bahame (2003), Faraja Kotta (2004), Nancy Sumari (2005), Wema Sepetu (2006), Richa Adhia (2007), Nasreen Karim (2008), Miriam Gerald (2009) na Genevieve Mpangala (2010).
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: