SERIKALI imeahidi kuwalipa mafao kwa muda wa maisha yao yote, watu wote waliopata ulemavu wa aina mbalimbali kutokana na milipuko ya mabomu iliyotokea katika ghala la silaha la Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Aprili 29, mwaka huu, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Wiliam Lukuvi, alisema watu hao watalipwa fidia kulingana na madhara yaliyowapata.

Bw. Lukuvi alisisitiza kuwa Serikali ipo pamoja nao kwamba na itawasaidia kuendesha maisha yao ya kila siku.

Alifafanua kuwa mafao watakayokuwa wakilipwa watu hao , yatajulikana baada ya wataalamu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kutoa mchanganuo wa kile wanachostahili kuwa wanalipwa kulingana na aina ya ulemavu waliopata.

"Wizara ya Afya ndio inahusika na kufanya hesabu, nimewaagiza watuletee idadi kamili ya watu waliopata ulemavu wa kudumu pamoja na mapendekezo yao," alisema Bw. Lukuvi.

Alisisitiza kuwa taarifa hiyo itaambatana na ile tathmini ya maafa itakayotolewa Juni 13, mwaka huu.

Bw. Lukuvi alisisitiza kuwa yupo makini kwa kuwa anaguswa na maafa yaliyowapata wakazi wa Mbagala.

Kuhusu vurugu zilizotokea wakati wa ugawaji misaada kwa waathirika wa mabomu, Bw. Lukuvi alisema kazi ya kusimamia ugawaji wa misaada hiyo ameachiwa Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Bw. Said Mkumbo.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: