RISALA YA RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI,
DK. AMANI ABEID KARUME, KUUKARIBISHA MWAKA MPYA 2009 AD, 1430 A.H., DISEMBA 31, 2009


BISMILLAHI RAHMAN RAHIM


Ndugu Wananchi,
Assalam Aleykum,
Naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Muweza kwa kutujaalia umri tukaweza kuuaga Mwaka wa 2008 Miladia na Mwaka 1429 Hijriya kwa salama na kuadhimisha kushuhudia kuingia Mwaka Mpya wa 2009 A.D., 1430 Hijriya kwa furaha. Tuna wajibu wa kumshukuru Mola kwa kutupa kheri hiyo tukiwa na salama na amani nchini mwetu.

Kumalizika kwa mwaka kunatupa fursa ya kufanya tathmini ya mafanikio yetu yote kwa jumla na pia kuzingatia upungufu uliokuwepo ili tufanye marekebisho. Pia, ni wakati unaofaa kuchunguza hali ya dunia kwa jumla na vipi inavyotuhusu. Kwa kufanya hivyo tutaweza kukabili Mwaka Mpya kwa matumaini na uhakika wa mafanikio.

Kwa upande wa nchi yetu, ni jambo la kufurahisha kuwa kwa jumla tulikuwa na mwaka wa mambo mengi ya kuridhisha na mafanikio katika sehemu mbali mbali. Katika mwaka tunaouaga tumeshuhudia maendeleo mema katika kustawisha uchumi wetu ambao unakadiriwa kukua kwa wastani wa asilimia sita. Ustawi huu umetokana na kuimarika kwa sekta za uchumi, zikiwemo kilimo, biashara, utalii na miundombinu, hasa ya barabara na mawasiliano. Katika mwaka huo, pia tumepiga hatua kubwa katika kukuza ustawi wa jamii, hasa katika sekta za elimu, afya pamoja na maji safi na salama. Aidha, tumekuwa na utulivu katika jamii ambao umechangia katika kutuletea maendeleo tuliyoyapata. Natoa shukurani kwa wananchi nyote kwa juhudi na ushirikiano wenu mkubwa uliosababisha mafanikio hayo. Tathmini kamili ya maendeleo yetu tutaitoa Inshaallah katika sherehe zetu za Mapinduzi ya Januari 1964. Leo nataka nigusie tu hali ilivyokua katika dunia yetu ambayo pia imetuathiri na sisi.

Kuanzia mwaka 2006 kulitokea upungufu wa chakula katika soko la dunia, hali ambayo ilikuwa mbaya zaidi mwaka 2008. Kutokana na hali hii, biashara ya vyakula vya nafaka kama ngano, mchele na mahindi ilikuwa ngumu kwa nchi kama yetu ambayo huagiza vyakula hivyo. Bei ya mahindi na ngano ilipanda mara tatu na ya mchele mara tano ya ilivyokuwa mwaka 2006/2007.

Shirika la Chakula Duniani, FAO, liliitisha mkutano maalumu wa viongozi wa nchi mbali mbali kujadili hali hiyo na kupitisha maazimio ya hatua za dharura za kuinusuru dunia. Nilihudhuria mkutano huo kwa niaba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwa upande wetu tulifanikiwa kupata ahadi za kusaidiwa kukuza kilimo chetu ili tupambane na hali hiyo ngumu ya chakula.

Wakati huo huo, bei ya mafuta ilipanda maradufu na kuathiri uchumi wa dunia kwa jumla. Nchi zetu pia ziliathirika ingawa tumemudu kuendesha shughuli zetu katika kipindi hicho kabla bei ya mafuta kushuka kwa kiasi fulani.

Ndugu Wananchi,
Wakati tatizo la upungufu wa chakula dunia halijamalizika, nusu ya pili ya mwaka 2008 tumeshuhudia mataifa yaliyoendelea yakipata matatizo makubwa ya uchumi. Umoja wa Mataifa umesema tatizo hilo ni kubwa tokea lile la mwaka 1930. Uchumi wa nchi hizo unatarajiwa kushuka kwa kiasi cha asilimia 1.5. Mataifa mengi yaliyoendelea yameshatoa sura za kutokuwepo ukuaji wo wote wa uchumi wao.

Matatizo hayo ya dunia, kwa vyo vyote vile, yana athari hata kwetu. Wataalamu wa uchumi wanaeleza kwamba athari ya kuporomoka uchumi wa nchi zilizoendelea inatarajiwa kuanza kuonekana mwaka 2009, hasa katika sekta za fedha, biashara na utalii.

Ndugu Wananchi,
Wakati tunaukaribisha Mwaka Mpya wa 2009, tuna jukumu la kujipangia maazimio ambayo yatatuwezesha kupambana kwa mafanikio ili tuepukane na matatizo hayo makubwa yanayoikumba dunia. Nimefarajika sana kwamba nchi yetu iliepukana na shida za upungufu wa chakula mwaka 2008. Hilo liliwezekana kutokana na hatua za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kudhibiti ushuru wa uagizishaji na kuwawezesha wafanyabiashara kuleta vyakula vya kutosha. Pamoja na hayo, hali hiyo pia ilichangiwa sana na juhudi za wakulima wetu kuongeza uzalishaji wa mazao ya vyakula vyengine. Napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru na kuwapongeza wakulima na wafanyabiashara wetu kwa juhudi zao zilizotunusuru na janga la upungufu wa chakula. Juhudi na moyo kama huo ndio utakaotuwezesha tufaulu vyema katika mwaka mpya.

Napenda kuwahimiza wakulima wetu kuendelea na bidii mkijua kuwa Serikali yenu kutokana na maazimio ya Shirika la Chakula Duniani na Mpango wetu wa Kupunguza Umasikini itapatiwa kila msaada unaowezekana.. Miongoni mwa msaada huo ni kuwapatia mbegu bora zilizofanyiwa majaribio na wataalamu wetu, mbolea kwa bei nafuu na mafunzo ya ukulima stadi ili waweze kujiendeleza. Haya ni katika maazimio yetu ya Mwaka Mpya, ambayo ni mongoni mwa Malengo ya Maendeleo ya Milenia.

Ndugu Wananchi,
Katika kupambana na uchumi dhaifu unaosambaa katika mataifa, sisi sote tunawajibika kujiweka vyema tusipigwe na dhoruba hizo. Miongoni mwa mambo ya kuazimia kufanya mwaka ujao ni kutunza matumizi yetu, kuepukana na ubadhirifu au utumiaji mbaya wa rasilmali zetu; kulinda mali za umma na kuhakikisha walipaji kodi wanawajibika ipasavyo na wakusanyaji wanafanya kazi yao kwa bidii zaidi na ufanisi mkubwa. Kutokana na msema maaarufu wa haba na haba hujaza kibaba, kwa hivyo kila hatua au kitendo chema cha mwananchi kitasaidia maendeleo ya taifa kwa jumla.

Utekelezaji wa maazimio hayo ya Mwaka Mpya pamoja na ushirikiano wa wananchi na washirika wetu wa maendeleo, utatuhakikishia uwezo wa kusalimika pakubwa na matatizo hayo yanayoikabili dunia. Natoa wito kwa kila mwananchi aelewe na akubali kikamilifu dhamana yake katika utekelezaji wa maazimio yetu. Hayo ndiyo yatakayopelekea kuwa na Mwaka Mpya wa mafanikio makubwa.

Wakati huo huo, tunaingia Mwaka Mpya, wakati zoezi la kutayarisha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura linaendelea. Tushirikiane sote kulikamilisha ili tufaulu kustawisha demokrasia na haki za watu wote kwa salama na amani.

Ndugu Wananchi,
Hali ya dunia inahitaji sote tushirikiane na tuungane inapohusu ustawi wa nchi yetu. Tunaweza kufanya hayo na ni wajibu wetu kuyafanya.

Natoa shukurani na pongezi kwa watumishi wa serikali, wafanyakazi viwandani, wafanyabiashara, wakulima na wavuvi kwa mchango wao mkubwa katika kutumikia nchi yetu mwaka uliopita.

Nakutakieni nyote Mwaka Mpya wenye kheri, baraka na mafanikio kwa kila mmoja wenu. Namuomba Mola Wetu Karimu atujaalie Mwaka wa Neema na Rehema zake nyingi; tuendeleze amani na utulivu; tukuze umoja na mshikamano wetu. Mungu atulinde na atunusuru na kila janga, Amin. Namuomba Mwenyezi Mungu ajaalie amani katika nchi ambazo kwa sasa hazina utulivu, hasa zilizo jirani nasi pamoja na nchi rafiki.

KHERI YA MWAKA MPYA
HAPPY NEW YEAR
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: