Msanii nyota wa kundi la muziki la TMK Wanaume Halisi Juma Kassimu ‘Sir Nature’ jana alifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Temeke akikabiliwa na tuhuma za kumbaka mwanafunzi (jina lake na la shule vinahifadhiwa).

Nature alisomewa mashitaka akiwa na mwenzake aitwaye Godwin Malima, mbele ya Hakimu mfadhiwi wa mahakama hiyo Bi. Hellen Riwa.

Akiwasomea mashitaka hayo mwendesha mashitaka wa mahakama hiyo Bw.Basall Pandisha alidai kuwa, mnamo Novemba mosi mwaka huu majira ya saa 1 jioni katika baa ya Sugeray Temeke Jijini Dar es Salam Nature na mwenzake huyo walimbaka kwa zamu msichana huyo mwenye umri wa chini ya miaka 18, huku wakielewa kuwa ni kinyume cha sheria.

Aidha, mwendesha mashitaka huyo alidai kuwa shitaka la pili ni kwa mtuhumiwa wa pili Bw.Godwin ambalo ni kumtorosha msichana huyo kutoka kwa wazazi wake bila ridhaa yao.

“Ulimtorosha msichana huyo bila ridhaa ya wazazi wake huku ukielewa kuwa ni kosa kumtorosha msichana bila idhini ya wazazi tena mwenye umri wa chini ya miaka 18,”alieleza mwendesha mashitaka huyo.

Hata hivyo, Nature na mwenzake walikana mashitaka hayo na waliachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti waliyokuwa wamepewa mahakamani hapo ambayo ni kuwa na mdhamini mmoja, mwenye hati ya nyumba, anayefanya kazi Serikalini au hati yeyote ya mali yenye thamani ya Shilingi Milioni 5.

Nature na mwenzake huyo walikamatwa Novemba 15 mwaka huu majira ya saa mbili ingawa waliachiwa kwa dhamana ambapo jana walifutiwa dhamana na kuwekwa chini ya ulinzi wa Polisi tena kisha kufikishwa mahakamani hapo majira ya saa sita mchana kwa gari maalum ya Polisi wakiwa chini ya ulinzi mkali.

Kesi yao inatarajiwa kusomwa tena Desemba 1, mwaka huu.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: