RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Amani Abeid Karume jana jioni aliungana na viongozi kutoka nchi mbali mbali za Afrika katika chakula cha jioni kilichoandaliwa na Rais wa Uganda Mhe. Yoweri Museveni kwa ajili ya sherehe za ufunguzi wa msikiti mkuu nchini humo.
Hafla hiyo ilifanyika Ikulu mjini Entebbe nchini Uganda ambapo ilihudhuriwa na viongozi hao akiwemo Rais wa Libya Mhe. Muammar Al Gaddafi ambaye ndiye mdhamini wa msikiti huo mkubwa katika eneo la nchi zilizo Kusini mwa jangwa la Sahara uliojengwa mjini Kampala.
Akiwakaribisha viongozi mbali mbali waliofika kwenye hafla hiyo Rais Museveni alitoa shukurani zake za dhati kwa ujio wa viongozi hao pamoja na kumpongeza Rais Karume kwa kujumuika pamoja katika hafla hiyo sambamba na uzinduzi wa msikiti huo.
Rais Karume ambaye amemuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete nae alipokea shukurani hizo.
Akizungumza na viongozi hao, Rais Museveni alitoa shukurani zake kwa Rais Gaddafi kwa ujenzi wa msikiti huo mkubwa ambao unaonesha ishara kubwa ya upendo kati ya wananchi wa viongozi wa Uganda na ndugu zao wa Libya.
Rais Musevani alisema kuwa msikiti huo utaimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya nchi mbili hizo na kusisitiza kuwa Uganda na Libya zina urafiki na udugu wa siku nyingi.
Alisema kuwa Waislamu wa Uganda wamefarajika kwa kiasi kikubwa kutokana na msaada wa Rais Gaddafi alioufanya kwa kuwajengea msikiti huo wa aina yake.
Rais Museveni alisema kuwa msikiti huo ambao ulianzishwa na Rais Iddi Amin mnamo mwaka 1972 utasaidia zaidi kuwaunganisha waislamu wa Uganda na hata waislamu kutoka nchi nyengine za ndani na nje ya Afrika.
Nae Rais Gaddafi alisema kuwa anafuraha kubwa sana kuona uhusiano na ushirikiano wa Uganda na Libya pamoja na nchi nyengine za Afrika unaimarishwa kwa kujenga misingi imara ya umoja katika nyanja mbali mbali ikiwemo kuimarishwa kwa dini ya Kiislamu nchini Uganda.
Alisema kuwa Libya nayo inathamni sana uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya nchi za Afika.
Rais Gaddafi alisema kuwa uislamu ni dini ambayo siku zote imekuwa ikiwaunganisha watu sambamba na kuimarisha umoja na mshikamano miongoni mwao.
Aidha, Rais Gaddafi alisema kuwa Mtume Muhammad ni kiongozi bora na kutokana na misingi madhubuti ya imani aliyoiweka ambayo imekuwa ikifuatwa na Waislamu hadi leo hii hivyo kuna ulazima wa kumkubuka na kumuenzi sambamba na kuiimarisha dini ya Kiislamu.
Rais Gaddafi alisema kuwa amefurahishwa kwa kuungana pamoja na viongozi mbali mbali waliohudhuria katika hafla hiyo akiwemo Rais Karume, Rais Ismail Omar wa Djibout, Rais Abdalla Yussuf Ahmed wa Somali, Rais Nkurunziza wa Burundi pamoja na viongozi wengine.
Msikiti huo unatarajiwa kuzinduliwa leo rasmi na Rais Gaddafi.

PICHANI NI RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WAA BARAZA LA MAPINDUZI MHE AMAANI ABEID KARUME,AKIMUWAKILISHA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANIO WA TANZANIA,JAKAYA MRISHO KIKWETE,PAMOJA NA MARAIS WA NCHI ZA AFRIKA WAKIWA KATIKA HAFLA YA CHAKULA CHA JIONI HUKO IKULU YA ENTEBE MJINI UGANDA, IKIWA NI SHEREHE ZA UFUNGUZI WA MSIKITI MKUBWA WA NCHI ZA ENEO LA JANGWA LA SAGHARA, UILIODHAMINIWAA NA RAIS WA LIBYA MUAMMAR GADDAFI, AMBAYE ATAKUWA MGENI RASMI KATIKA SHUGHULI HIYO.

PICHA NA RAMADHAN OTHMAN,UGANDA.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: