Makamu wa Rais Dk. Ali Mohamed Shein (wa tatu kutoka kushoto) na mkewe mama Mwemapamoja na waziri wa Afya Pfo David Mwakyusa jana alitembelea kusini mwa India katika jimbo la Bangalore na kuongea na wanafunzi wa Tanzania huko. Hapa makamu na ujumbe wake katika picha ya pamoja na wanafunzi hao.

Makamu wa Rais Dk. Ali Mohamed Shein amewataka wanafunzi kutoka Tanzania wanaosoma nchini India kuishi kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu za nchi hiyo.

Akisalimiana na wanafunzi wanaosoma katika vyuo vya Bangalore na Karnataka nchini India Dk. Shein amesema hatua hiyo itasaidia kuwawezesha kuishi vizuri na wenyeji wao na hivyo kufanikisha lengo lao la kupata taaluma.

“Muendelee kuishi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za nchi hii..jengeni mazingira ya kuishi vizuri na wenyeji wenu. Mjiepushe na mambo yasiyo ya msingi, bila ya hivyo mtakosa mliyoyajia”, alisema Makamu wa Rais.

Katika mkutano huo Makamu wa Rais alielezea pia jitihada mbalimbali zinazofanywa na serikali katika kuimarisha sekta ya elimu nchini Tanzania na kuwataka wasome kwa bidii na wakimaliza wakumbuke kurudi nyumbani kuja kulitumikia Taifa.

Katika Risala zao wanafunzi hao kutoka vyuo hivyo vilivyoko Bangalore na Karnataka walizungumzia matatizo ya ukosefu wa fedha kiasi kwamba wakati mwingine wanashindwa kusaidiana inapotokea mmoja wao amepata matatizo.

Hata hivyo wanafunzi wanaosomeshwa kwa udhamini wa serikali wametaja matatizo yanayowakabili ni pamoja na ukosefu wa fedha za mafunzo kwa vitendo jambo ambalo linafanya shahada zao kuwa na mapungufu.

Wanafunzi hao walimweleza Makamu wa Rais tatizo jingine ni kukosekana kwa fedha za malazi kwa kuwa Bodi ya mikopo ya elimu ya juu haijaleta fedha hizo kwa mwaka huu wa 2007/2008.

Aidha waliiomba serikali iwawekee bima ya afya ya uhakika kwani bima waliokatiwa na ubalozi mwaka 2005/2006 ilikuwa dhaifu kifedha kiasi kwamba wamekuwa hawapati huduma za uhakika wanapougua.

Akizumzungumzia hoja ya mikopo Dk. Shein aliwahakikishia wanafunzi hao kuwa atalifuatilia suala hilo na pia aliwataka wampe ushirikiano balozi wa Tanzania nchini India ili aweze kuwatumikia kwa ufanisi katika kutatua matatizo yao mbalimbali yanayowakabili.

Wanafunzi waliiomba serikali kuhakikisha kuwa Tovuti ya Taifa inarusha habari za kila siku kutoka Tanzania badala ya kuziachia tovuti za binafsi.

Kwa mujibu wa Balozi wa Tanzania nchini India Eng. John Kijazi jumla ya wanafunzi wa kitanzania 954 wanasoma nchini India ambapo kati yao 96 wanagharimiwa na serikali.

Akiwa hapa Bangalore mbali na kusalimiana na wanafunzi wa kitanzania Dk. Shein alitembelea kampuni ya Biocon ya kutengeneza madawa, kiwanda cha Software Technology Park na hospital ya Manipal. Aidha wakati wa jioni alikuwa na mazungumzo na Gavana wa Karnataka. Leo Jumamosi Makamu wa Rais anakwenda Mumbai kuendelea na ziara yake nchini India .

Habari kwa hisani ya Penzi Nyamungumi – Bangalore, India .
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: