Kwa siku kadhaa sasa, mitandao ya kijamii na baadhi ya vyombo vya habari - ndani na nje ya Tanzania vimekuwa vikiandika na kutangaza habari za kile kinachodaiwa kuwa tuhuma dhidi yangu zilizotolewa na baadhi ya Wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA).

Tuhuma hizo ambazo kimsingi ni mkakati wenye ajenda ya siri nyuma yake, umekuzwa na hata kufikia hatua ya baadhi ya Waheshimiwa Wabunge kukwamisha baadhi ya shughuli za Bunge hilo mjini Kigali, Rwanda.

Kuvunjika kwa kikao hicho kulitokana na madai ya baadhi ya wabunge waliokuwa wakishinikiza Bunge linichukulie hatua kwa kuniondoa kwenye Ujumbe wa Kamati ya Uongozi ya EALA.

Madai yao ni pamoja na lugha mbaya kwa baadhi ya wabunge, kuwatukana baadhi ya marais wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, ulevi wa kupindukia na kufanya fujo, kuvunja chupa ndani ya ndege na hatimaye kufungwa pingu wakati wa ziara ya baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wa EALA nchini Ubelgiji.

Madai yote haya hayana ukweli wowote na yanalenga kuniharibia jina na sifa yangu ya utendaji kazi wangu katika Bunge la Afrika Mashariki. Lengo kuu la shutuma hizi ni kunivunja nguvu na ari ya kutetea maslahi ya nchi yangu na Afrika Mashariki kwa ujumla. Shutuma hizi zinadhihirisha waziwazi chuki kubwa walioyonayo maadui zangu kwa vile daima nilisimama kidete kuhakikisha Spika wa Eala Dr. Margaret Zziwa haondolewi madarakani kwani hoja hiyo haikuwa na maslahi ya Tanzania na ilikuwa ni kinyume na malengo ya EAC.

Kwa tuhuma nzito kama hizo nilitarajia kupata mawasiliano rasmi ya kimaandishi kutoka kwa uongozi wa bunge kutaja shutuma zote dhidi yangu na ni nani anayelalamika. 

Hilo halikufanyika Kwa mfano madai ya ulevi wa kupindukia, kufanya fujo na kuvunja chupa ndani ya ndege ni kosa kubwa la jinai (ugaidi). Madai haya yalipaswa kuwa na ushahidi kwa sababu si rahisi abiria afanye fujo ndani ya ndege, halafu aachwe hivi hivi bila kuchukuliwa hatua za kisheria. Safari yetu ya Ubelgiji tulitumia usafiri wa Shirika la Ndege la KLM. Iwapo tuhuma hizi zingekuwa na ukweli shirika hilo lisingesita kunichukulia hatua za kisheria.

Tuhuma kama hizi zinapashwa kupelekwa kwenye Kamati ya Uongozi ya Bunge (EALA Commission) ambayo ina mamlaka ya kushughulikia jambo hilo. Spika aliitisha kikao cha kamati hiyo lakini kilikosa akidi kwa makusudi kabisa kutoka kwa baadhi ya wajumbe.

Lengo na makusudi ya kutohudhuria kikao hicho ilikuwa ni kupeleka hoja hiyo moja kwa moja bungeni ili nichukuliwe hatua za kinidhamu bila ya mimi kama mtuhumiwa kusikilizwa.

Baada ya kikao cha Kamati ya Uongozi kukosa akidi, hatua iliyofuata ni kwa Mbunge kutoka Uganda, Dora Byamukama, (aliyeshindwa kwenye uchaguzi wa uspika 2012 Juni mwaka 2012 dhidi ya Dr. Zziwa) kuwasilisha hoja kwenye kikao cha Bunge, akipendekeza niadhibiwe kwa kuvuliwa Ujumbe wa Kamati ya Uongozi.

Katika hilo, hekima ilitawala kuwa sikutendewa haki kwani sikupewa malalamiko kimaandishi; badala yake hoja hiyo ililetwa jumla. Kwa hilo la kukosa kunipa mashitaka kimaandishi, wabunge wengi wa Tanzania waliamua kutoka nje ya Bunge kuonyesha msimamo wao dhidi ya upungufu wa ukiukwaji wa mtuhumiwa kutopewa kimaaandishi mashtaka dhidi yake na fursa ya kujitetea (Natural Justice).

Baada ya kukwama kwa hoja hiyo, baadhi ya wenyeviti wa Kamati na baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Uongozi walitangaza kujiuzulu nafasi zao. Walifanya hivyo ili kushinikiza Bunge linivue Ujumbe katika Kamati ya Uongozi.

Hata hivyo, katika hatua ya kushangaza, Wenyeviti wawili kati ya waliotangaza kujiuzulu wameonekana wakiendesha vikao vya kamati zao katika miji ya Kigali, Rwanda na Nairobi, Kenya. 

Ni Mhe. Dora Byamukama (kamati ya sheria) na Mhe. Martin Nduwimana (Kamati ya Maendeleo ya Jamii) ambaye alishiriki kama mwenyekiti katika mkutano wa EAC iliofanyika Nairobi kuanzia tarehe 5-7 Novemba. (Hii nimeshuhudia kwa macho yangu maana nilihudhuria mkutano huo).

Wakati viongozi hawa walitangaza hatua ya kujiuzulu baada ya tuhuma za uzushi dhidi yangu kukosa mashiko, inashagaza kuwaona wakiendelea na nyadhifa zao kana kwamba hawakuutangazia umma juu ya uamuzi wao.

Ikumbukwe kwamba umebaki mwezi mmoja tu wa kipindi cha viongozi wote wa Kamati ya Uongozi na Kamati zote za bunge la Eala kumaliza kipindi cha uongozi ili wachaguliwe wengine baada ya kutumikia nafasi hiyo kwa miaka miwili na nusu (kuanzia Juni 2012). Kwa lugha nyingine viongozi hawa wameamua kujiuzulu ikiwa zimebaki wiki chache tu kabla ya timu mpya kuchaguliwa.

MIGOMO
Ukweli ni kwamba migomo kama hii ni mwendelezo wa migomo iliyodumu kwa makusudi baada ya azma yao ya kumng’oa Spika wa Bunge, Dr. Zziwa kushindwa. Hawakupata sahihi za kutosha kutoka kwa wabunge wa Tanzania. Kwa sababu hiyo, katika Kikao cha Bunge kilichofanyika Agosti, mwaka huu jijini Dar es Salaam wabunge wengi kutoka Rwanda na Burundi walisusia na hivyo kusababisha akidi kutotimia.

Hapa anayetafutwa si Shy-Rose Bhanji, bali Spika Dr. Zziwa kwani wabunge kadhaa wameshupaa ili ang’olewe kwenye kiti hicho. Wabunge hao wanajua mimi siungi mkono jambo hilo, na kwa sababu hiyo wameamua kunizushia uongo ili wana Afrika Mashariki waone sina uhalali wa kumtetea Mheshimiwa Spika Zziwa. Msimamo wangu ni kwamba bado sioni sababu za msingi zinazowasukuma wabunge kadhaa kutaka kumng’oa Spika Zziwa.

Si mimi pekee ninayemtetea Spika Zziwa. Wapo wengine. Tofauti yangu ni kwamba nilisimama kidete muda wote kumtetea; ndani ya Kamati ya Uongozi ya Bunge, ndani ya vikao vya bunge na nje ya Bunge; hatua ambayo sina shaka ndio iliyowakasirisha na kuamua kunizushia uongo.

Wabunge wa EALA tumepewa dhamana kubwa kwa ajili ya kuimarisha utangamano wa wananchi wa Afrika Mashariki; lengo kuu likiwa kuinua hali zao za maisha. Ni kwa sababu hiyo, chombo hiki kinapaswa kuwa na watu wenye weledi na wenye kujua kutumia vema muda na rasilimali ambazo zinatokana na jasho la walipakodi wa Afrika Mashariki.

Haiingii akilini, na kwa kweli si kuwatendea haki wananchi wa Afrika Mashariki kwa Wabunge wa EALA kutumia muda na fedha za walipakodi kujadili uzushi, kugomea vikao na kupoteza muda wakitaka kumng’oa Spika na kuendekeza mivutano isiyokoma. Haya siyo tuliyotumwa na wana Afrika Mashariki.

Rai yangu kwa wabunge wenzangu ni kurejea kwenye maudhui ya kuanzishwa kwa EAC na kuwapo kwa Bunge la EALA kuanzia kwenye kikao cha bunge kinachotarajiwa kufanyika jijini Nairobi, Kenya.

Kwa kufanya hivyo, tutajua tuna deni kubwa la kuwaletea wananchi wetu maendeleo.
Migongano ya kisiasa au tofauti zetu za kimtazamo zisiwe chanzo cha kuvurugika kwa utangamano ambao umeonyesha kuwa tukiwajibika vizuri, wananchi zaidi ya milioni 140 wa EAC watapata mafanikio makubwa.

HITIMISHO
Makusudio ya tuhuma hizi ni kunidhalilisha na kunipunguzia nguvu, ari na kasi ya utendaji kazi wangu kama Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki. Lakini pia ni kutaka kunivunja nguvu ili nisiendelee kumtetea Spika Mheshimiwa Dk. Zziwa na pia kujenga hofu na woga mkubwa kwa wabunge wengine ambao wana mtazamo na msimamo kama wangu.

Kuna ushahidi tosha kwamba mchango wangu ni kwa Tanzania kwanza na Afrika Mashariki kwa jumla. Ninawaomba wananchi waendelee kuwa na imani katika juhudi na mchango wangu; na kupuuza uzushi na tuhuma ambazo hadi sasa wazushi wameshindwa kuzithibitisha.

Kwa kuwa tuhuma hizi si tu kuwa ni mbaya kwangu, bali hata kwa nchi yangu; iwapo wabunge hawa watashindwa kuthibitisha madai yao, sitosita hata kidogo kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria.

Shy-Rose Bhanji
Mbunge wa Afrika Mashariki-Tanzania
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: