Shughuli za mauzo na manunuzi zilirejea rasmi jana mjini Mtwara, baada ya huduma hizo kusimama kwa siku tatu kutokana na vurugu zilizotokea kuanzia Alhamisi baada ya kusomwa hotuba ya Wizara ya Nishati na Madini na wana-Mtwara kubaini kuwa suala lao la gesi halijapewa umuhimu unaostahili. Picha na Abdallah Bakari.

MTWARA. MKUU wa vikosi vya aridhini wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Meja Jenerali SM Kijuu amewahakikishia ulinzi wafanyabiashara hao, baada ya kukutana na uongozi wa Chama cha Wafanyabiashara Sokoni (Wabisoco) jana asubuhi, kufuatia wafanyabishara hao kudai kuendelea kusitisha biashara zao kwa kuhofia usalama.

Katibu wa Wabisoco, Saidi Namata alisema kuwa wafanyabiashara hao wamekubaliana kufungua biashara zao, baada ya makubaliano ya kulinda eneo hilo na askari wa JWTZ.

“Sisi wafanyabiashara tulikuwa tayari kuendelea kusitisha huduma kutokana na hali ya usalama kuwa mbaya, alipokuja kiongozi wa jeshi na kutuhakikishia kuwa dhamana ya ulinzi itakuwa chini yao tulikubaliana,” alisema Namata.
Alisisitiza: “Kama ulinzi ungekuwa mikononi mwa polisi, katu tusingefungua.

Polisi wenyewe ndiyo hawa wanaovunja maduka na kuiba, kwa kuwa dhamana hii imebebwa na wanajeshi hatuna shaka, tunaomba wafanyabiashara wengine wafung ue biashara zao.”

Tangu juzi magari ya matangazo yamekuwa yakipita mjini Mtwara na kuwatangazia wananchi kuendelea na kazi zao kama kawaida kwa kuwa ulinzi umeimarika, huku askari wa JKT na JWTZ waliosheheni silaha wakizunguka mitaani.

Wakati huo Waziri Mkuu Mizengo Pinda amewasili Mtwara jana jioni na kukutana na viongozi wa mkoa.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: