Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari Loyola ya jijini Dar es Salaam wakifuatilia mada mbalimbali ndani ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Shule ya Sekondari Loyola.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Bi. Lilian Liundi akizungumza na wanahabari kwenye maadhimisho ya Siku ya Wanawake Shule ya Sekondari Loyola.
Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari Loyola wakionesha ubunifu wa mavazi katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Shuleni hapo.
---
Na Mwandishi wa Thehabari.com
KAIMU
Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Bi. Lilian
Liundi amesema wanawake wanaweza kuwa viongozi wazuri na mfano wa kuigwa
katika maeneo mbalimbali endapo watajengewa mazingira na kuandaliwa
mapema tangu wawapo shuleni.
Bi. Liundi ambaye
pia ni Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya TGNP ametoa changamoto
hiyo leo katika Shule ya Sekondari ya Loyola ya jijini Dar es Salaam
alipokuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku ya mwanamke shuleni
hapo.
Akizungumza na umati wa wanafunzi
wasichana wa shule hiyo na wageni anuai waalikwa, alisema tafiti nyingi
zilizofanywa zinaonesha kuwa wasichana wanapoandaliwa mazingira mazuri
ya elimu wanafanya vizuri ukilinganisha na wavulana.
Aidha
aliongeza kuwa kwa sasa zipo shule zinazochukua wasichana pekee ambazo
zimekuwa zikifanya vizuri zaidi jambo ambalo linaonesha wazi mazingira
mazuri yakijengwa jamii hii inaweza kuinuka na kuwa mfano mzuri.
Alisema
kwa sasa vishawishi na changamoto anuai zilizopo katika shule nyingi
ndio kikwazo kwa wanafunzi wa kike kufanya vizuri, hali ambayo
ikifanyiwa kazi kiufasaha mabadiliko kimafanikio kwa kundi hilo yanaweza
kutokea.
Hata hivyo alisema tafsiri
iliyojengeka ya kwamba wanafunzi wa kike wanaogopa masomo ya sayansi si
sahihi kiuhalisia, kwani mazingira ambayo wanafunzi hawa wanakumbana
nayo ndio kikwanzo katika mafanikio yao kimasomo.
“Mfano
shule nyingi za kata ni za kutwa wanafunzi hasa wasichana wanakaa mbali
na shule, wanalazimika kutembea umbali mrefu kwenda na kurudi
shuleni…wanakumbana na changamoto nyingi njiani hivyo wanajikuta
wanashindwa kufanya vizuri au kukatishwa kabisa masomo yao,” alisema Bi.
Liundi.
Aliongeza kuwa eneo kama hili, vyombo husika
vikiangalia sheria na sera zinazojenga mazingira mazuri kwa makundi
yote, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha rasilimali zilizopo zinatumika
vizuri wasichana wanaweza kuingia katika ushindani kwa fursa zilizopo.
Kwa
upande wake mwanafunzi Grace Ntambi wa kidato cha tano wa shule hiyo
aliiomba serikali kuendelea kutoa elimu kwa mikoa ambayo bado
inaendeleza mila potofu za kumbagua mtoto wa kike ikiwa ni pamoja na
kuelemea kwenye mfumo dume, ili kuangamiza vitendo hivyo.
“Na
hii ianzie pia katika ngazi za familia kuna kila sababu ya kuondokana
na mila potofu za kwamba mtoto wa kike hana haki ya kupata elimu kama
ilivyo kwa mtoto wa kiume…tuwatie moyo wasichana kwani wanawea,”
alisema mwanafunzi huyo.
Katika hafla hiyo pia
TGNP ilipata fursa ya kutoa mada mbalimbali za masuala ya wanafunzi
kujitambua kwa hatua anuai ikiwa ni pamoja na kutoa ushuhuda ya kwamba
wanawake wanaweza wakiamua kufanya hivyo kwa kila hatua wanayopiga.
*Imeandaliwa na Mtandao wa Thehabari.com (www.thehabari.com).
Toa Maoni Yako:
0 comments: