Na Luppy
Kung’alo wa Jeshi la Polisi Dodoma.
Watu wanne wa Kundi la “lambalamba” wanashikiliwa
na jeshi la Polisi Mkoani Dodoma kwa
kijifanya wanafichua wachawi katika vijiji mbalimbali katika maeneo ya wilaya
za Chamwino, Kongwa na Mpwapwa. kumbe wanawatapeli wanavijiji kwa lengo la
kujipatia fedha
Akizungumzia tukio hilo Kamanda
wa Polisi mkoa wa Dodoma, Kamishna msaidizi wa Jeshi la Polisi Bw. David Misime
amesema uchunguzi wao umebaini kuwa vitu wanavyojifanya kuvitoa ndani ya nyumba
au maduka ya watu, kuwa ni wao wenyewe hutuma wenzao kuvipandikiza na baadaye hujifanya wamevikuta kwenye nyumba ya mtu
anayetuhumiwa kuwa ni mchawi.
Aliwataja waliokamatwa wakiwa
wanajiandaa kuendesha shughuli za lambalamba katika kijiji cha Vilundilo
Wilayani Kongwa kuwa ni mwanaume mmoja Mkombozi Salehe, na wanawake watatu ambao
ni Hadija Tupa, Joyce Nhembelo na Siwema Kwaeli, ambao walikuwa ni kwa ajili ya
kuwapikia lambalamba hao.
“Wanawake waengine
hutafutwa kwa ajili ya kulala nao jambo ambalo ni hatari kwani mbali ya kwamba
ni kinyume cha sheria na unyanyasaji wa kijinsia pia upo uwezekano mkubwa wa
kuambukizwa magonjwa ikiwepo UKIMWI.” Alisisitiza Bw. David Misime.
Aidha alitoa wito kwa wananchi
kuelewa kuwa wanatapeliwa fedha zao na
hao watu waliobuni mradi wa kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kwani
wamejionea wenyewe kuwa wanachangishwa fedha kabla ya kuwaita na hata
wanaodaiwa kuwa wachawi, hudaiwa kiasi cha fedha.
Kamanda David Misime
alisema kuwa shughuli wanazoendesha kundi hilo la Lamba lamba ni kinyume cha
sheria za nchi na ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binanadamu kwa kuwaita baadhi
ya watu kuwa ni wachawi kwa lengo la kujipatia fedha.
Mkuu huyo wa Jeshi la
Polisi Mkoani Dodoma alisema Upelelezi zaidi unakamilishwa ili wafikishwe
mahakamani wakati wowote, pamoja na Ufuatiliaji
wa lambalamba wengine waliokimbia pamoja na viongozi vijiji wanaoshirikiana nao
unaendelea.
Wakati
huo huo Polisi Mkoani
Dodoma inamshikilia kwa mahojiano IDDI S/O RAMADHANI PANDAUYAGA @ NGOSHA,
MSUKUMA, Mkazi wa DODOMA MAKULU baada ya kulalamikiwa na wananchi wengi kwa
kujipatia fedha kwa njia udanganyifu kuwa anawauzia viwanja.
Kamanda Misime amesema hadi
sasa mtu huyo ameshatapeli zaidi ya Tshs. 24,537,000/= kuanzia mwezi Agosti,
2012. Kwa kuwarubuni watu kuwa viwanja hivyo ametumwa na wafanyakazi wa CDA
kuviuza.
Bw. David Misime alitoa wito
kwa wananchi wasikubali kurubuniwa kuwa wanauziwa kiwanja na kutoa fedha bila
kuthibitisha kiwanja hicho kama kipo na ni halali.
Toa Maoni Yako:
0 comments: