Baada ya miezi mitatu ya mchuano mkali hatimaye mshindi wa shindano la kuimba la Epiq Bongo Star Search atapatikana leo katika fainali kali inayofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee.

Mshindi atajinyakulia shilingi milioni hamsini pamoja na mkataba wa kurekodi kutoka kwa wadhamini pekee wa shindano hilo kampuni ya simu za mikononi ya Zantel.

Washiriki walioingia kwenye fainali hizo ni EBSS06: Nsami Nkwabi, EBSS07: Nshoma Ng’hangasamala, EBSS09: Salma Abushiri, EBSS11: Wababa Mtuka (Dar) na EBSS12: Walter Chilambo (Dar).

Wasanii watakaoburudisha ni Rich Mavoko, Omi Dimpoz, Ben Paul, Lina, Amini, Mzee Yusuf, Haji Ramadhan, Mwasiti, Ditto, Laila Rashid, Linex na Barnaba.    

Akizungumzia fainali hizo, jaji mkuu wa shindano hilo, Madam Ritha Paulsen, aliwashukuru watanzania kwa ushirikiano waliowapa toka shindano limeanza mpaka leo wanahitimisha kwa fainali.

 ‘Kama mlivyoona shindano hili toka lilipoanza mwaka huu limekuwa la kimataifa zaidi, hivyo tarajieni fainali za kipekee na zitakazoweka rekodi kwenye tasnia ya burudani na ni matarajio yetu kwamba mshindi wa usiku huu atafanya vizuri kwenye muziki’ alisema Madam Ritha.

Kwa upande wake Afsa Biashara mkuu wa Zantel, bwana Sajid Khan alisisitiza utayari wa kampuni yake katika kuwaendeleza vijana wa kitanzania kufikia ndoto zao lakini aliomba pia wadau wengine wa sanaa kuwapa washirikiano washiriki wote.

‘Zantel, pamoja na kumpa mshindi zawadi ya milioni hamsini lakini pia tutampa mkataba wa kurekodi, na washiriki wengine watapewa nafasi ya kurekodi wimbo mmoja mmoja lakini juhudi hizi zitafanikiwa ikiwa tutapata ushirikiano wa kutosha kutoka kwa wadau’ alisema Khan.

Shindano hilo limekuwa likirushwa hewani na kituo cha runinga cha ITV, lilianza mwezi wa sita kwa kufanya usaili mikoani, ambalo mwaka huu lilienda mikoa nane-Mbeya, Dodoma, Mwanza, Tanga, Dar es Salaam, Zanzibar, Lindi pamoja na Arusha.

Kwa mara ya kwanza pia shindano hilo liliweza kufanya usaili kwa njia ya simu ili kuwapa nafasi vijana zaidi ambao hawakufikiwa na majaji.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: