SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC) lina mpango wa kuondoa
nyumba ndogo katika maeneo yenye thamani kubwa yaliyojengwa holela mijini na
badala yake kujenga maghorofa kukidhi mahitaji ya makazi, Mkurugenzi Mkuu wa
NHC, Bw. Nehemia Kyando Mchechu ametangaza.
Akimkaribisha Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuzindua ujenzi wa
nyumba za makazi eneo la Medeli mjini Dodoma ,
Bw. Mchechu alisema mpango huo utaanzia eneo la Mikocheni “A” jijini Dar
es Salaam .
Watakaokutwa kwenye maeneo watapata haki ya kumilikishwam
baadhi ya nyumba katika maghorofa yatakayojengwa na nyumba nyingine za ziada
zitakazobaki Shirika litaziuza kwa wateja wengine, alisema.
“Kwa hivi sasa tunajadiliana na Manispaa na Wizara ili
kutekeleza mpango huo ambao ni sehemu ya mkakati mkubwa wa Shirika kujenga
nyumba nchini kote na kuziuza badala ya kujenga na kupangisha kama
ilivyo sasa,” alisema.
Maeneo mengine ya jiji la Dar es Salaam yatakayohusika na
mpango huo ni Msasani na Kawe ambayo ni ya thamani kubwa lakini yamevamiwa na
kujengwa bila ya mpangilio mzuri.
Kuna Sheria ya Utoaji Miliki za Sehemu ya Majengo (The Unit
Tittle) inayowezesha kila mtu kuwa na miliki ya sehemu yake katika nyumba ya
ghorofa iliyopitishwa hivi karibuni.
Katika uzinduzi wa jana, Waziri Mkuu aliweka jiwe la msingi
kwa maghorofa mawili yenye nyumba 40 ambayo yamekamilika. Kutajengwa maghorofa
yatakaokuwa na nyumba 290 hapo Medeli, ambazo kati yake 240 zitapangishwa kwa
ajili ya Chuo Kikuu cha Dodoma
kilicho jirani na 150 za kuuzwa, ambayo mojawapo imekwishauzwa kwa Sh. Milioni
99.
Hatua nyingine ya mpango wa NHC wa kuendeleza makazi nchini
ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010, ni uendelezaji
wa majengo yanayomilikiwa na Shirika hilo na kuyaendeleza maeneo mengine mapya.
Bw. Mchechu alisema Mamlaka ya Ustawishaji wa Makao Makuu Dodoma (CDA)
imeipatia NHC eneo la ekari 264 nje kidogo ya mji wa Dodoma ili kujenga majengo ya makazi.
Akihutubia kwenye uzinduzi huo, Waziri Mkuu aliwataka
wakandarasi wa ndani ya nchi ambao ndiyo pekee waliopata kazi ya kujenga nyumba
hizo na NHC wasitie aibu kwa kushindwa kutimiza wajibu wao ama sivyo
watafukuzwa.
“Msichakache. Tekelezeni kazi zenu vizuri, watu wawasifie na
mjenge uzoefu, vinginevyo itakuwa aibu na Mchechu (Mkurugenzi wa NHC)
atawafukuza,” Mhe. Pinda alisema.
Toa Maoni Yako:
0 comments: