Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Wakazi wa maeneo mbalimbali ya Kigamboni wamejikuta wakikosa mawasiliano ya uhakika baada ya daraja muhimu linalounganisha maeneo yao kuzama maji kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha.
Daraja hilo, linalotumika kuunganisha maeneo ya Kibada, Mji Mwema, Cheka, Buyuni, Dege na Geza, limeripotiwa kufunikwa na maji, hali iliyosababisha wakazi kubaki kama wamejitenga na maeneo mengine.
Mashuhuda wamesema hali hiyo imekuwa ikijirudia mara kwa mara wakati wa mvua kubwa, jambo linaloathiri shughuli za kiuchumi, usafiri na hata huduma za dharura kwa wakazi wa maeneo hayo.
“Wakati maji yanapoongezeka, daraja linapotea kabisa. Inakuwa kama sisi tumeachwa kama kisiwa,” alisema mmoja wa wakazi wa eneo hilo.
Wakazi hao wameeleza kuwa daraja hilo ni kiungo muhimu kwa maisha yao ya kila siku, likitumika kusafirisha wanafunzi, wafanyabiashara pamoja na wagonjwa wanaohitaji huduma za haraka.
Aidha, wameitaka serikali pamoja na mamlaka husika kuchukua hatua za haraka kuboresha miundombinu hiyo ili iweze kuhimili hali ya mvua na kuzuia madhara yanayojirudia kila mwaka.
Baadhi yao wamependekeza kujengwa kwa daraja la kudumu na lenye kiwango cha juu zaidi, ili kuhakikisha usalama wa watumiaji pamoja na kuimarisha mawasiliano kati ya maeneo hayo.
Hadi sasa, mamlaka husika hazijatoa tamko rasmi kuhusu hali hiyo, huku wakazi wakiendelea kuishi kwa tahadhari na matumaini ya kupatiwa suluhisho la kudumu.



No comments:
Post a Comment