Pages

Wednesday, 20 August 2025

Vyombo vya Habari Vahimizwa Kuanzisha Madawati ya Sheria kuelekea Uchaguzi Mkuu

Na Vero Ignatus, Arusha.

Vyombo vya habari nchini vimetakiwa kuanzisha na kuendeleza madawati ya sheria yatakayowasaidia waandishi wa habari kuepuka makosa ya kisheria kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025.

Wito huo umetolewa jana Agosti 20, 2025, Jijini Arusha na Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Ernest Sungura, wakati wa mafunzo ya msaada wa kisheria kwa waandishi wa habari wa mkoa wa Arusha.

Sungura alisema madawati hayo yatakuwa msaada muhimu kuhakikisha habari zinazochapishwa hazivunji sheria, sambamba na kuwasaidia waandishi kuepuka udhalilishaji au uchochezi unaoweza kuwaingiza matatani.

“Maisha yako yana thamani kubwa kuliko kazi unayoifanya. Kwa kuwepo na dawati la ushauri wa kisheria, mwandishi au chombo cha habari kitaepuka kuingia matatani,” alisema Sungura.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Arusha (APC), Cloud Gwandu, alisema mafunzo hayo yamekuja wakati muafaka, kwani yatawasaidia wanachama wake kufanya kazi kwa uangalifu zaidi hasa katika kipindi cha uchaguzi.

Aidha, aliwataka waandishi waliopata mafunzo hayo kuwa mfano wa kuigwa kwa kuzingatia sheria na weledi katika uandishi.

Naye mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Julius Msagati, alisema elimu hiyo imemuwezesha kufahamu haki na wajibu wake kikatiba, pamoja na umuhimu wa kuandika habari kwa kuzingatia matakwa ya kisheria.

“Mafunzo haya yametupa mwongozo sahihi. Yamekuja wakati sahihi na kwa kundi sahihi,” alisema Msagati.

Kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2020 ya mwenendo wa madhila kwa waandishi na vyombo vya habari iliyotolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT), jumla ya waandishi na vyombo vya habari 40 walikumbwa na madhila mbalimbali, huku Jiji la Dar es Salaam likiongoza na Arusha kushika nafasi ya pili.

No comments:

Post a Comment