Pages

Friday, 1 August 2025

CCM yarekebisha Mchakato wa Kura za Maoni kwa Wagombea Udiwani

Na Mwandishi Wetu, Dodoma.

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa kimetoa maagizo mapya kuhusu mchakato wa kura za maoni kwa wagombea udiwani katika kata zote nchini kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025.

Katika taarifa rasmi kwa umma iliyotolewa tarehe 1 Agosti 2025 na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Itikadi, Uenezi na Mafunzo CPA Amos Gabriel Makalla, chama hicho kimetangaza kuwa wagombea wote waliopitishwa na Kamati za Siasa za Mikoa warejeshwe ili kupigiwa kura za maoni.

“Wagombea wote wa udiwani wa kata waliopitishwa na Kamati za Siasa za Mikoa warejeshwe ili wapigiwe kura za maoni,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Aidha, CCM imeelekeza kuwa hata wagombea waliokuwa kwenye orodha ya awali iliyowasilishwa kwa makatibu wa mikoa nao warejeshwe kwenye mchakato huo kwa ajili ya kupigiwa kura.

Hatua hiyo imekuja baada ya kikao cha Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kilichofanyika Alhamisi ya tarehe 31 Julai 2025, kujadili kwa kina malalamiko yaliyowasilishwa kutoka mikoa mbalimbali kuhusu mchakato huo.

“Kikao hicho kimefuta maelekezo yote ya awali na kuelekeza utekelezaji wa maagizo haya mapya kwa makatibu wote wa mikoa nchini,” ilisisitiza taarifa hiyo.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa utekelezaji wa maagizo mapya unapaswa kuzingatiwa kwa umakini ili kuhakikisha haki na usawa katika mchakato wa ndani ya chama kuelekea uchaguzi mkuu.

No comments:

Post a Comment